Jumatatu, 25 Mei 2015

Madiwani Walia Na Ndoa FEKI Za Walimu......Wadai Upungufu Wa Walimu Vijijini Unasababishwa Na Walimu Wa Kike Kughushi Vyeti Vya Ndoa


BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, wamesema tatizo la upungufu wa walimu kwenye shule za msingi zilizopo vijijini kunachangiwa na walimu hasa wa kike kutaka kufundisha mjini.

Walisema baadhi ya walimu wa kike wamekuwa wakighushi vyeti vya ndoa ili kuonesha wameolewa na kuwafuata waume zao mijini jambo linalozorotesha jitihada za Serikali kumaliza tatizo la walimu kwani baadhi ya shule za vijijini zina walimu hadi wawili.

Madiwani hao waliyasema hayo mwishoni mwa wiki kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo ambapo Diwani wa Kata ya Lusanga, Sesiwa Mhando, alidai halmashauri ilitenga sh. milioni 30 kwa ajili ya walimu kupelekwa shule za vijijini; lakini hadi sasa hajui mchakato huo umekwamia wapi.

"Tatizo la walimu kwenye shule za msingi linatokana na walimu kujazana mijini hasa wa kike wakiwa na ndoa   bandia, madiwani tulitenga sh. milioni 30 ili zitumike kupeleka walimu vijijini lakini sijui mchakato huo umeishia wapi," alihoji.

Kwa upande  wake, Kaimu Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wilayani humo, Stuart Kuziwa, alisema tatizo la walimu ni la kitaifa likiwemo la kujazana mijini lakini hata shule zilizopo mjini nazo zina upungufu wa walimu.

"Hata shule za mjini nazo zina upungufu wa walimu, tumeomba kupatiwa walimu 230 kwa miaka mitatu mfululizo, hilo linaweza kumaliza shida ya walimu katika shule za msingi," alisema.

Diwani wa Kata ya Bwembera, Kapteni mstaafu Tito Haji, alisema moja ya shule za msingi kwenye kata yake ina walimu wawili.

"Kwenye Kamati ya Fedha,mlidai tatizo la walimu limekwisha sasa iweje leo mnatueleza kuwa tatizo la walimu bado lipo Muheza, Shule ya Msingi Msowelo ina walimu wawili lakini mjini walimu wamejaa," alisema Kapteni Tito.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Amir Kiroboto, alisema madiwani wasilalamikie tatizo la walimu kujaa mijini bali waangalie idadi ya wanafunzi kwani shule nyingi za mjini zina wanafunzi wengi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni