Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kufanya mkutano wa dharura hii leo kuijadili Burundi baada ya jenerali mwandamizi wa jeshi nchini humo kutangaza kumpindua Rais Pierre Nkurunzinza kutoka madarakani.
Ufaransa ndiyo imeitisha kikao hicho cha dharura ambacho kitafanyika hii
leo punde tu baada ya wanachama wa baraza hilo la usalama la Umoja wa
Mataifa kuijadili Iraq.
Hapo jana Meja Jenerali Godefroid Niyombare ambaye alikuwa mkuu wa
shirika la ujasusi nchini Burundi, alitangaza kuwa utawala wa Rais
Pierre Nkurunzinza umepinduliwa na jeshi kutoka madarakani kwa kukiuka
matakwa ya raia.
Wakati wa tangazo hilo la kupinduliwa kwa serikali, Nkurunzinza alikuwa
Tanzania kuhudhuria mkutano wa viongozi wa jumuiya ya nchi za Afrika
Mashariki uliotishwa na mwenyekiti wa jumuiya hiyo Rais wa Tanzania
Jakaya Kikwete kuujadili mzozo huo wa Burundi.
Niyombare aliagiza viwanja vyote vya ndege na mipaka yote ya ardhini ya
Burundi kufungwa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametoa
wito wa dharura kwa pande zote nchini Burundi kuonyesha utulivu na
kujizuia kufuatia jaribio la mapinduzi ya serikali dhidi ya Rais
Nkurunzinza.
Msemaji wa katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephanie Dujarric
amesema Ban amesisitiza haja kwa viongozi wote wa Burundi kudumisha
amani na uthabiti katika taifa ambalo limekumbwa na matukio ya ghasia
mbaya katika kipindi cha nyuma.
Marekani imewataka waburundi kuweka silaha chini kufuatia ripoti za
kupinduliwa kwa serikali ya Nkurunzinza na msemaji wa ikulu ya Rais wa
Marekani Josh Ernest amesema nchi yake inafuatilia matukio yanavyojiri
Burundi kwa makini na wasiwasi.
Marekani imesema bado inamtambua Nkurunzinza kuwa kiongozi rasmi wa
Burundi lakini inamshinikiza kuheshimu katiba ya taifa hilo na mikataba
ya amani ilyofikiwa mwaka 2000 kwa kutogombea muhula wa tatu.
Hatma ya Nkurunzinza haijulikani baada ya ofisi ya Rais hapo jana
kutangza anarejea nyumbani kutoka mkutano wa viongozi wa Afrika
Mashariki nchini Tanzania na alitarajiwa kulihutubia taifa.
Lakini ndege yake haikuweza kutua mjini Bujumbura na badala yake ilirudi Tanzania baada ya viwanja vya
ndege kufungwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni