Jumatano, 17 Septemba 2014

Hatimaye Mhe Freeman Aikael Mbowe Amechaguliwa Tena kuwa mwenyekiti wa Chadema Taifa kwa kupata kura 789 sawa na asilimia 97.3 ya kura zote. Aliyeshinda nafasi ya Makamu mwenyekiti Bara ni Profesa Abdallah Safari kwa kupata kura 775 sawa a asillimia 95 na nafasi ya Makamu mwenyekiti Zanzibar ameshinda Mh Saidi Issa Mohamedi kwa kupata kura 645 sawa na asilimia 79.                     



Freeman Mbowe akiwasalimia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema.
Freeman Mbowe ameshinda tena nafasi ya Uenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa baada ya kupata jumla ya kura 789 huku mpinzani wake Ngambaranyela Mongatero akipata kura 20.
 
 
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema wakifuatilia mkutano huo.
Mbowe ameshinda nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.


TUTENGENEZE KATIBA INAYOLENGA KUTATUA MATATIZO YA WANANCHI WETU KWA MIAKA 50 IJAYO. Prof:Mwandosya.

MJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba Mhe. Prof. Mark Mwandosya ameeleza kuwa mpaka ifikapo mwaka 2055 Tanzania itakuwa imeachana na umaskini katika nchi ya uchumi wa kwanza endapo kutakuwa na dhamira ya dhati hususani kuwa kuandika Katiba yenye kuleta nafuu kwa watanzania kwani kila kitu kwa Waafrika kinawezekana pasipo kuwa na Wazungu.
 
 Prof. Mwandosya alisema hayo jana wakati akichangia mjadala wa katiba ndani ya Bunge Maalum, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuwa na katiba itakayozingatia vipaumbele ambavyo vinaweza kumkwamua mwananchi wa kawaida kuondokana na umasikini na kuliinua Taifa kiuchumi.
 
 Mhe. Mwandosya amesema kuwa kuhusu changamoto na kero zinazohusu mambo ya Muungano, katiba imejaribu kuzizingatia karibia zote, huku akieleza kuwa hali ya Muungano ni imara na itaendelea kuwa imara.
 Ili kufanikisha nchi inapiga hatua baada ya kuwa na Katiba bora, Mhe. 
 
Mwandosya amefafanua kuwa, watumishi wote wa Umma hawana budi kuliletea tija Taifa hili kwa kuwa misingi imewekwa ndani ya rasimu ya katiba  na kusisitiza kuwa Mtumishi wa Umma sio mtawala na mambo yanayohusu miiko na maadili ya mtumishi huyo yenye kumtumikia mwananchi serikali Katiba imeweza kuyazungumzia.
 
“Tumezungumzia kuhusu rushwa ambaye ni adui wa haki, kwamba hili tulitambue katika Katiba ili katika Sheria likasimamiwe vilivyo na pia tumezungumzia pia wale wanaouhujumu uchumi”, alisema Mhe. Mwandosya.
 Kuhusu haki za vijana, Mhe. Mwandosya ameeleza kuwa katika Rasimu ya Katiba wamezungumzia juu ya haki za vijana, haki za walemavu, haki za wazee, pamoja na haki za watoto, huku akiwashangaa baadhi ya wajumbe walioko nje ya bunge hilo wanapotoa shutuma kuwa wanapoteza wakati kana kwamba hawazungumzii mambo yanayowahusu wananchi.
 
 “Nawaomba wananchi watusikilize na wayazingatie haya tunayoyasema”. Alisema Mhe. Mwandosya.
 Akizungumzia kuhusu Vyombo vya Usalama, amesema kuwa Katiba inawalinda na kuwatambua viongozi wa usalama, ambapo sheria inawapa haki hata baada ya kustaafu ili wakaweze kuishi maisha bora kwa kuchukua dhamana kubwa, hivyo kwa dhamana hiyo viongozi hao wanapostaafu wanatakiwa kujiepusha na masuala ya kisiasa kwasababu.
 “Usalama wa Taifa, Jeshi, Polisi, Magereza na Uhamiaji, hawa tunawatengezea mambo mazuri sana wanapostaafu, kwahiyo tafadhari sana mkishatoka tusaidieni, toeni ushauri lakini mkijiingiza katika siasa na mafaili yetu huku mmeyashika hamtutendei haki”, alisema Mhe. Mwandosya.
 
 
 Aidha, ameomba kuwepo na Randama kwani hiyo inaandikwa katika lugha ambayo mwananchi anaweza kuisoma tofauti na katiba kwani hiyo inaandikwa kwa lugha ya kisheria, kwahiyo amependekezo kuwepo na randama kwa ajili ya wananchi.
 Mwandosya ameongezea juu ya suala la amani kuwa ni jambo kubwa sana, amewananga watu wenye tabia ya kutaka wananchi kuandamana wakapigwe risasi hao ni watu wasioitakia mema nchi, hivyo amewaasa wananchi walipinge kwa nguvu zao zote kuhusu suala hilo.
 
 “Nina ushauri kwa viongozi wenye kutaka wananchi wakapigwe risasi na Polisi, naomba watangulie wao wajipige risasi, unapotaka kuwa Shujaa anzia kwanza wewe mwenyewe, usiwapeleke vijana ambao ni matumaini ya nchi yetu, ndugu zangu hili jambo siyo la busara hata kidogo na wananchi mnapokwenda kuandamana, vijana mseme mnaandamana kwa nini? Kwasababu gani? Na kwa misingi gani na kwasababu ya nani? Ukishajibu haya maswali kwakweli mtaona nchi yetu kuwa ni nzuri sana, nchi ya amani”, alisisitiza Mhe. Mwandosya.

MJUMBE WA BUNGE MAALUM LA KATIBA AWATAKA BAADHI YA VIONGOZI KUTII SHERIA.

 
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba,Mhe. Hamad Rashid amewaomba viongozi  kuheshimu na kutii sheria.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mhe. Rashid wakati kikao cha Arobaini cha Bunge hilo, kinachoendelea  mjini  Dodoma cha kujadili sura zote 15 zilizobakia za Rasimu ya  Katiba Mpya, ikiwa ni mjadala wa mwisho.
“Hakuna dhambi mbaya ya kuamrisha mtu kuvunja sheria. Ninaomba sana ndugu zangu na viongozi wenzangu tutii sheria. Ndugu zangu tutulie tuendeshe nchi . Hii nchi ina bahati ya ajabu,” alisema Rashid huku akisisitiza kuwa ina Rais wa ajabu ambaye anaweza kumsikiliza mtu hata ambaye anampa amri.
 
Mhe. Hamad aliwataka watu wasicheze na dola, huku akitolea mfano yeye na wenzake 18 waliwahi kuwekwa ndani. Hivyo aliwaasa viongozi  wenzake wasicheze na Serikali, bali waitii.
Bunge hilo, ambalo linaendelea kwa mujibu wa sheria, ambapo baadhi ya wajumbe waliwataka wabunge wenzao kuendelea na kazi waliyotumwa na wananchi  ya kuhakikisha Katiba  inayopendekezwa inapatikana Oktoba 4,mwaka huu.

Jumatatu, 8 Septemba 2014

Tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania Kuhusu Mchakato wa Katiba



Sisi, wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, tuliokutana tarehe 27 hadi 28 Agosti, 2014, Dar es salaam , tumepata fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika Rasimu ya pili ya Katiba na mjadala unaoendelea katika Bunge Maalum la Katiba. Baada ya mjadala wa kina, tunatoa tamko letu kama ifuatavyo:
  • Tunaipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikusanya Maoni ya WANANCHI kuhusu mabadiliko hayo na kutuletea Rasimu yenye maoni mengi ya Watanzania bila kujali dini zao, upande wa Muungano walikotoka, hali zao za kimaisha, jinsi na kabila.
  • Pia tunaipongeza Tume kwa kuandaa nyaraka na kumbukumbu mbalimbali kama Randama, Nyaraka zenye maoni ya wananchi, picha, tafiti mbalimbali na hata orodha ya watu walioshiriki kutoa maoni katika Tume. Tume pia iliweza kuandaa Tovuti iliyokuwa na kumbukumbu za Tume na Maoni yote yaliyotolewa. Kazi hii ni ushahidi kuwa Tume iliandaa Rasimu kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuzingatia maoni ya WANANCHI.
  • Tume imedhihirisha kuwa, ilitenda KIZALENDO na, kwa mantiki hiyo, wajumbe wote bila kujali vyama vyao, dini zao na upande wa Muungano walikotoka, waliweza kujadili kwa uwazi na kweli na mwisho wakaridhiana katika kila Ibara iliyopendekezwa. Hili linatufundisha kuwa Katiba ni MARIDHIANO na si jambo la maslahi ya kisiasa, bali ni suala la maslahi ya WANANCHI.
  • Tunaamini kuwa kila Mjumbe wa Kamati ya kukusanya maoni ya WANANCHI aliheshimu kiapo chake na hivyo kufanya kazi waliyokabidhiwa kwa uaminifu na uadilifu na ya kwamba hawakushawishiwa au kupokea rushwa kutoka kwa kundi, dini au chama chochote cha siasa wakati wa zoezi hili.

Baada ya Tume kuwasilisha Rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba, Taifa likaanza kushuhudia “uasi wote na uovu wa wanadamu wapingao kweli kwa uovu” (Warumi 1:18). Katika mijadala ya Bunge Maalum la Katiba (BMK) yakaanza kujitokeza mambo mengi yasiyo ya maslahi kwa WANANCHI, na ukiukwaji wa sheria na kanuni. Mambo kadhaa yanadhihirisha hili:
  • Tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifungwa bila sababu za msingi kutolewa wakati mchakato unaendelea. Hali hii imefanya zile nyaraka na kumbukumbu zilizoandaliwa kwa ajili ya rejea na kuwezesha mjadala wa Rasimu ya Katiba kuendelea katika mwanga na ufahamu wa nyaraka hizo kutowezekana kabisa. Kwa sababu hiyo, tumeona Bunge Maalumu la Katiba likiendelea kupotosha takwimu na taarifa mbalimbali ambazo WANANCHI hawawezi kuzipata kwa ajili ya kuoanisha baina ya kinachojadiliwa Bungeni na kilichomo katika Rasimu na viambatanisho vyake vyote. Tunajiuliza jambo hili limefanywa na nani na kwa maslahi ya nani?
  • Bunge la Katiba limeshindwa kusimamia Kanuni kama ambavyo zilipendekezwa na kuridhiwa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Kushindwa huku kusimamia kanuni kumesababisha vurugu ndani ya Bunge Maalumu na kumekwamisha matarajio ya wananchi kupata Katiba bora ya nchi yetu. Matumizi ya ubabe na wingi wa Wabunge wa Chama Tawala (CCM), badala ya Kanuni za Bunge na maridhiano, kumefanya mchakato wa Katiba kuhodhiwa na Chama Tawala dhidi ya maslahi ya WANANCHI.
  • Mijadala katika Bunge Maalumu la Katiba imekuwa ya kejeli, matusi, vitisho, ubabe na kupuuza hata kupotosha maoni yaliyotolewa na Wananchi kwa Tume. Hali hii imelifanya Bunge Maalumu la Katiba kupuuzwa na hivyo kupoteza heshima na hadhi yake. Matokeo yake baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakaamua kususia vikao vya bunge na wengine kuendelea, bila kukumbuka kuwa KATIBA NI MATOKEO YA TENDO LA MARIDHIANO NA SI SUALA LA MASLAHI YA KIKUNDI CHA WATU WACHACHE.
  • Hatua iliyofikiwa ni dhahiri, Mjadala wa BMK unaoendelea umeondoa kwa kiasi kikubwa maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu muundo wa Muungano, kupunguza mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge, ukomo wa ubunge, n.k., na kuwezesha maoni na maslahi ya Chama Tawala kwa uongozi wa kikundi cha wanasiasa wachache wasio na uaminifu na uadilifu wa kutosha kuwekwa kama mapendekezo ya Katiba mpya kwa nia ya kulinda maslahi binafsi au ya makundi na kuhalalisha ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na maadili ya uongozi bora.
Baada ya kujadili na kuona haya na mengine mengi, Jukwaa la Wakristo Tanzania lina maoni yafuatayo;
1. Kwamba Serikali (Wizara ya Katiba na Sheria) irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zote kwa ajili ya wananchi kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza na kujadili Rasimu ya Katiba kwa uwazi.
2. Kwamba maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauliwa na Chama Tawala. Hivyo basi, Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea lijadili na kuboresha tu maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na sio kufanya mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977.
3. Kwamba mchakato wa Katiba usimamishwe ili kupisha majadiliano, maelewano na maridhiano muafaka, uchaguzi mkuu na wa serikali za mitaa. Na mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977 yafanyike kuwezesha chaguzi kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka kifungu kitakacholinda Rasimu ya pili na kumtaka kiongozi ajaye kuendelea na mchakato wa Katiba.
4. Kwamba baada ya Bunge Maalum la Katiba kuanza shughuli zake tena, Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi kwa mujibu wa kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia ubabe na kiburi cha wingi wa wajumbe wa Chama cha Mapinduzi katika Bunge la Katiba.
5. Kwamba wananchi waendelee kusoma na kujadili maoni yaliyoko katika Rasimu ya pili ya Katiba, na kufuatilia kitakachokuwa kinajadiliwa kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga kura ya maoni wakiwa na uelewa wa kutosha kabisa kuhusu ni nini kipo kwenye “Katiba inayopendekezwa”. Wananchi pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa nia ya kuwawezesha kupiga kura ya maoni.
6. Kwamba tunaomba Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihuishwe na kupewa mamlaka kisheria ili kuiwezesha kujibu maswali yanayojitokeza na kutoa ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa jumla hadi Katiba Mpya itakapokamilika na kukabidhiwa rasmi.
Jukwaa la Wakristo Tanzania na Watanzania wote wanaoitakia nchi yao mema, tunakuomba Mheshimiwa Rais kwamba AMANI ya nchi yetu sasa imo mikononi mwako hasa katika kipindi hiki cha kuandikwa kwa Katiba Mpya. Tunakuomba uahirishe mchakato unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali za kuanzisha sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri vibaya mshikamano, umoja na amani ya Taifa letu.
Ifahamike kuwa WANANCHI wa Tanzania wako juu ya Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi. Kwa mantiki hiyo, tunakuomba uepushe WANANCHI wa Tanzania kuhamasishwa kukikataa Chama cha Mapinduzi kwa kuwa tu Chama hicho kimeyapuuza na kimekataa Maoni yao waliyotoa kwa dhati baada ya kuaswa na kuhimizwa kufanya hivyo na viongozi wa nchi.
“Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutabakari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenyekuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao”. (Rejea Warumi 1: 28-32)

IKUMBUKWE KUWA RASIMU YA PILI YA KATIBA NI WARAKA HALALI NA RASMI NA NDIYO MAWAZO YA WATANZANIA NA TUNAHIMIZA KUWA KATIBA NI YA WANANCHI NA INAHITAJI MARIDHIANO NA SIO UBABE.
Imetolewa leo Agosti 28, 2014
Na MKUTANO WA JUKWAA LA WAKRISTO
Tanzania Episcopal Conference (TEC)      
The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT)   
Christian Council of Tanzania (CCT)         
The Seventh Day Adventists (SDA)

 

Jumamosi, 6 Septemba 2014

Mwanasheria mkuu wa Zanzibar ajitoa katika uandishi wa Katiba



Taarifa ambazo bado hazijathibitishwa ni kwamba mwanasheria mkuu wa Zanzibar amemwandikia barua spika wa bunge la katiba kumtaarifu kujitoa katika timu aliyoiteua kuandika katiba baada ya vifungu kupitishwa na wabunge ambapo kwa kiasi kikubwa wamepingana na rasimu yenye maoni ya wananchi kitu kinachomfanya mwanasheria mkuu huyo kujitoa kwakuwa ni dhambi kuondoa maoni ya wenye nchi yao wananchi.
................................................. 

Dodoma. Kuna dalili hali si shwari ndani ya Bunge Maalumu la Katiba baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kujiuzulu ujumbe wa Kamati ya Uandishi wa Katiba inayopendekezwa.

Habari za uhakika zilizopatikana jana bungeni mjini Dodoma, zinaeleza kuwa kigogo huyo wa SMZ amemwandikia barua Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta akimwarifu juu ya uamuzi wake huo.

Kamati hiyo ndiyo moyo wa Bunge hilo katika kuandika vifungu, ibara na sura za rasimu kulingana na mapendekezo ya kila kamati na baada ya majadiliano na mwisho inawajibika kuandika Katiba itakayopendekezwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

Kujiengua kwake ni pigo kwa Bunge Maalumu, kwani kunapunguza uhalali wa Katiba itakayopendekezwa kwani Othman akiwa Mwanasheria Mkuu wa upande huo wa Muungano ndiye anayepaswa kuwa kinara wa kulinda masilahi ya Zanzibar wakati wa uandishi wa Katiba inayopendekezwa.

Jana Othman alilithibitishia gazeti hili kuhusu kujiuzulu kutoka kwenye kamati hiyo, lakini akakataa kueleza sababu zilizomsukuma kuchukua uamuzi huo akitaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu atafutwe kwani barua yake ya kujiuzulu ameikabidhi kwake.

“Ni sahihi kwamba nimejiuzulu…hizo sababu ndiyo siwezi kukutajia maana kwa mujibu wa taratibu za Bunge Maalumu zinapaswa kuzungumzwa na Mwenyekiti maana barua yangu ya kujiuzulu anayo yeye,”alisema Othman alipozungumza na gazeti hili kupitia simu yake ya mkononi jana.

Hata hivyo, Sitta alipotafutwa jana, alikataa kuzungumza lolote juu ya taarifa hizo akisema hawezi kufanya mahojiano na mwandishi asiyemfahamu kwa njia ya simu.

“Kwanza sikujui halafu unataka nifanye mahojiano kwenye simu? Mimi sipo (Dodoma), nipo Dar es Salaam ninarudi Jumatatu niliondoka huko (Dodoma) mara tu baada ya kipindi cha asubuhi,” alisema Sitta.

Kwa upande wake, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad, alipotafutwa alisema hajaiona barua hiyo ya Othman, lakini kwa utaratibu, mjumbe anayetaka kuchukua uamuzi kama huo humwandikia barua mwenyekiti ndipo ishuke chini.

“Mimi bado sijapata taarifa hiyo, labda atakuwa amewasilisha kwa mwenyekiti akishaipata ndiyo inaletwa huku kwangu,”alisema Hamad.

Alisema kwa sababu nafasi hizo ni uteuzi unaofanywa na mwenyekiti na kanuni ziko kimya kuhusiana na idadi ya wajumbe katika kamati, mwenyekiti ndiye mwenye uamuzi wa kuteua mtu mwingine ama kuacha.


Chanzo: Mwananchi