Jumapili, 3 Novemba 2013

Matokeo ya Mtihani wa Darasa la Saba 2013 02/11/2013

 

Imeelezwa kuwa ufaulu wa mtihani wa kumaliza darasa la saba kwa mwaka 2013 umepanda kwa masomo yote kwa asilimia 19.89 ikilinganishwa na ilivyokuwa kwa mwaka uliopita.

Kwamba, wakati mwaka jana wahitimu waliopata asilimia 100 walikuwa asilimia 30.72, mwaka huu wameongezeka kuwa asilimia 50.61. Pia, somo ambalo watahiniwa hao wamefaulu zaidi katika mtihani wao ni  Kiswahili ambapo ufaulu ni 
asilimia 69.06 huku wakiwa wamefeli zaidi kwenye somo la Hisabati ambalo ufaulu upo chini kwa asilimia 28.62.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde alisema wanafunzi 427,606 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013 huku kiwango cha udanganyifu kikizidi kudhibitiwa hivyo kupungua.

Alisema NECTA imefuta matokeo yote ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa watahiniwa 13, ambao walibainika kufanya udanganyifu kwenye mtihani au kurudia pasipo ruhusa ya Baraza. Watahiniwa waliofutiwa mwaka jana ni 293.

Alisema kati ya wanafunzi hao, 844,938 waliofanya mtihani huo wamepata alama zaidi ya 100 katika alama 250: “Idadi hiyo ni sawa na asilimia 50.61. Kati yao wasichana walikuwa 208,227 (sawa na asilimia 46.68) na wavulana 219,379 sawa na asilimia 55.01,” alisema.

Dk. Msonde alisema katika ufanyaji wa mtihani huo, pia walikuwepo watu wenye ulemavu, ambapo wasichana walikuwa 219 na wavulana 257.

Alisema matokeo hayo yatapelekwa maeneo yote husika ili mchakato wa upangaji shule ukifanyika kwa watahiniwa wote waliofaulu mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi.

Kuhusu usahihishaji mitihani, Dk. Msonde alisema ili kujiridhisha na usahihi wa zoezi la usahihishaji wa kutumia mfumo wa kompyuta (Optical Mark Reader - OMR), sampuli za karatasi 20,795 za majibu ya watahiniwa wa shule 200 kutoka wilaya 48 zilichukuliwa kutoka shule za mikoa tisa ya (Iringa, Kagera, Shinyanga, Manyara, Njombe, Mbeya, Morogoro, Katavi na Tanga) na kusahihishwa kwa mkono: “Ulinganifu baina ya alama za watahiniwa zilizopatikana kwa kusahihishwa kwa mkono na zile zilizotokana na usahihishaji wa mfumo wa kompyuta ulifanyika na kubaini kompyuta ilikuwa sahihi,”alisema.

Amesema makosa yaliyojitokeza katika karatasi zilizosahihishwa kwa mkono ni kuweka pata pale ambapo kuna kosa ama kuweka kosa pale ambapo kuna pata, makosa ambayo kwenye usahihishaji wa kutumia kompyuta hakuwepo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo alisema shule binafsi zimeongoza katika matokeo hayo kwa kila somo.

Alisema katika somo la Kiswahili, shule binafsi wamepata asilimia 98 wakati za Serikali asilimia 68, na kwa Kingereza shule binafsi asilimia 99 na Serikali 33. Kwa somo la Maarifa ya Jamii, shule binafsi asilimia 86 Serikali 52 , Hisabati shule binafsi asilimia 81 na Serikali 27 na somo la Sayansi, shule binafsi asilimia 84 na Serikali 46.

Matokeo ya dalasa la saba yaliyopachikwa hapo juu pia yanapatikana katika tovuti za:

  1. www.necta.go.tz
  2. www.edu.udsm.ac.tz
  3. www.matokeo.necta.go.tz
  4. www.moe.go.tz