Jumapili, 26 Aprili 2015

WATU 20 WAKAMATWA NA POLISI KWA KUMSHUSHIA KIPIGO ASKARI POLISI HUKO MOROGORO


WATU 20 wamekamatwa na Polisi baada ya kumjeruhi askari aliyekuwa doria. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alisema watu hao 20 wanatuhumiwa kumpiga na kitu butu kichwani Askari Polisi mwenye namba F 3328 Cpl Ramadhani akiwa kwenye doria na mwenzake.

Pia kamanda huyo alisema Polisi inamshikilia mkazi wa Mawenzi mjini hapa, Dikanyo Ramadhani (29) kwa kupatikana na kete 87 za dawa za kulevya aina ya heroin ambazo thamani yake haikuweza kujulikana mara moja.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa Aprili 23, mwaka huu majira ya saa nne usiku katika maeneo ya Soko kuu la Manispaa ya Morogoro.

Alisema Polisi waliokuwa doria maeneo hayo walimtilia shaka mtu huyo na baada ya kumpekua kwenye mifuko yake ya suruali walimkuta akiwa na kete hizo 87.

Akizungumzia tukio la kupigwa askari, Kamanda huyo alisema watu 20 wakazi wa Mindu na Sangasanga, Manispaa ya Morogoro walimshambulia kwa kumpiga na kitu butu kichwani askari wa jeshi hilo mwenye namba F 3328 Koplo Ramadhani.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, askari huyo baada ya kupigwa na watu hao alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro ambako amelazwa na anaendelea vizuri na matibabu.

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 23, mwaka huu majira ya saa 4: 45 asubuhi eneo la Mindu, barabara kuu ya Morogoro- Iringa, Manispaa ya Morogoro, ambapo pikipiki isiyofahamika namba za usajili iliyokuwa ikiendeshwa na Juma Abasi (18), mkazi wa Mindu kuligonga gari lenye namba za usajili T 953 AQF aina ya Isuzu Tipper iliyokuwa ikiendeshwa na Joseph Laurent (28) , mkazi wa Modeco.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo pikipiki hiyo iliyokuwa ikitokea Mindu Bwawani kuelekea barabara ya Iringa, mwendeshaji wake alipowaona askari Polisi wawili waliokuwa doria maeneo hayo wakiwa na pikipiki, aligeuka ghafla na kuingia barabarani bila kuchukua hadhari na kuigonga gari hiyo iliyokuwa ikitokea Morogoro mjini kuelekea Sangasanga na kusababisha majeraha kwa mpanda pikipiki huyo.

Kamanda huyo wa Polisi wa mkoa alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa mwendesha pikipiki huyo kuingia barabarani bila kuchukua tahadhari.

Hata hivyo alisema ajali hiyo ilishuhudiwa na askari hao waliokuwa doria na pikipiki maeneo hayo na hivyo walifika eneo la ajali ili kutoa msaada na katika harakati hizo za kutoa masaada ndipo askari Koplo Ramadhani alipopigwa na kitu butu kichwani na watu waliotokea eneo hilo na kuanguka chini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni