Jumatatu, 13 Aprili 2015

MTOTO ALIYEKUFA MWAKA JANA AFUFUKA...WATU WAFURIKA KUJIONEA MAAJABU HAYO HUKO KIBAMBA JIJINI DAR


Wakazi wa Kibamba nje kidogo ya jiji la Dar es salaam jana walifurika nyumbani kwa Emmanuel Joseph kushuhudia maajabu ya tukio la kufufuka kwa mtoto anayedaiwa kufariki dunia mwezi Agosti mwaka jana.
Mtoto huyo mwenye umri wa mwaka mmoja inadaiwa alizikwa katika makaburi ya Mlongazila na alifariki Agosti 7 baada ya kuugua gafla na kuishiwa damu.
Mtoto huyo anadaiwa kurudishwa akiwa hai na Juma Nakochinya (33) maarufu kwa jina la Bino, mkazi wa eneo la Pandambili mkoani Dodoma ambaye hutibu kwa njia ya maombi.
Akisimulia tukio hilo, mama wa mtoto  huyo, Hellena Mtoro, alisema ilikuwa siku ya Jumamosi majira ya saa 11:00 jioni ambapo mwanawe akiwa na umri wa miezi tisa alizidiwa ghafla na kumkimbiza hospitali ya Mbezi kwa matibabu.
Alisema baada ya kufika hospitalini hapo, vipimo vilionyesha ameishiwa damu hivyo alihamishiwa hospitali ya Tumbi, iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Madaktari walijitahidi kadiri ya uwezo wao kutafuta mishipa ya damu maeneo tofauti ya mwili ikiwamo kichwani, cha ajabu mishipa ilikuwa ikionekana lakini ilikuwa inavimba, wakati madaktari wakihangaika, ilipofika saa 6:00 usiku alifariki dunia,” Mtoro,
Alisema baada ya kuzika siku tatu baadaye walielekea Dodoma kwa ajili ya kumaliza msiba na kurudi Dar es Salaam.
“Ukweli ni kwamba kifo cha mtoto wangu kilikuwa sio cha kawaida, hivyo tulianza maombi na mume wangu, tulikuwa tunasali kwa Nabii Flora Peter, ambaye baada ya kumweleza mazingira ya kifo hiki, alimuweka kwenye maombi na kututaka tumpelekee picha yake,”
“Baada ya maombi alitueleza kuwa anamuona mtoto wetu yupo hai na anaamini atarudi siku moja. Tuliendelea na maombi na siku moja nilikutana na mama Mariamu ambaye baada ya kumwelezea kifo cha mtoto wangu, aliniambia kuna kijana anaitwa Bino ambaye anaweza kumrudisha kama alikufa kichawi,”
Alisema mama huyo alimpa namba ya mtu huyo na alipowasiliana naye, Bino alimtaka ashike Sh. 100.
“Nilifanya hivyo na baada ya dakika tano tukiwa bado hewani, alinijulisha kuwa mtoto wangu anamuona yupo hai hivyo akanitaka niende kesho yake Dodoma kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo ya kumrudisha,”
Hellena alisema siku iliyofuata alisafiri kuelekea Dodoma na aliwasili saa 10:00 jioni ambapo alienda moja kwa moja kwa mganga huyo.
“Saa 1:00 jioni Bino alichukua mwiko, ungo na kinu, vifaa anavyovitumia kwenye kazi yake. Ungo aliuweka chini na akaanza kusoma dua kisha nikamuona mtoto amekaa ndani ya ungo ule, nilishtuka sana baada ya kumwona akiwa hana hata nguo, amechafuka na aliyechoka,” alisema.
Alisema baada ya tukio hilo, mtoto alibaki kwa mganga huyo kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi.
Alisema alikaa kwa mganga huyo kwa muda wa siku mbili na kurudi Dar es Salaam na kumuacha mtoto huko kama alivyotakiwa.
“Jana aliletwa na Bino ili aje kutusalimia kwa kweli nashukuru Mungu kwa sababu hali ya mwanangu inaendelea vizuri, afya yake ipo vizuri, ” alisema.
Baba wa mtoto huyo, Joseph, alisema kuwa tukio hilo ni la kwanza na la aina yake kwenye ukoo wao na kwamba lilipotokea hakuna aliyeamini hadi walipomuona mtoto.
Alisema baada ya mtoto wake kuletwa, majirani ambao walishiriki kwenye msiba wake, walishtuka na kujaa nyumbani kwake kitendo ambacho kiliwalazimu kwenda polisi kutoa taarifa ya kile kilichotokea.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni