Wakazi
wa Kibamba nje kidogo ya jiji la Dar es salaam jana walifurika nyumbani
kwa Emmanuel Joseph kushuhudia maajabu ya tukio la kufufuka kwa mtoto
anayedaiwa kufariki dunia mwezi Agosti mwaka jana.
Mtoto
huyo mwenye umri wa mwaka mmoja inadaiwa alizikwa katika makaburi ya
Mlongazila na alifariki Agosti 7 baada ya kuugua gafla na kuishiwa damu.
Mtoto
huyo anadaiwa kurudishwa akiwa hai na Juma Nakochinya (33) maarufu kwa
jina la Bino, mkazi wa eneo la Pandambili mkoani Dodoma ambaye hutibu
kwa njia ya maombi.
Akisimulia tukio hilo, mama wa mtoto huyo, Hellena Mtoro,
alisema ilikuwa siku ya Jumamosi majira ya saa 11:00 jioni ambapo
mwanawe akiwa na umri wa miezi tisa alizidiwa ghafla na kumkimbiza
hospitali ya Mbezi kwa matibabu.
Alisema
baada ya kufika hospitalini hapo, vipimo vilionyesha ameishiwa damu
hivyo alihamishiwa hospitali ya Tumbi, iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
“Madaktari
walijitahidi kadiri ya uwezo wao kutafuta mishipa ya damu maeneo
tofauti ya mwili ikiwamo kichwani, cha ajabu mishipa ilikuwa ikionekana
lakini ilikuwa inavimba, wakati madaktari wakihangaika, ilipofika saa
6:00 usiku alifariki dunia,” Mtoro,
Alisema baada ya kuzika siku tatu baadaye walielekea Dodoma kwa ajili ya kumaliza msiba na kurudi Dar es Salaam.
“Ukweli
ni kwamba kifo cha mtoto wangu kilikuwa sio cha kawaida, hivyo tulianza
maombi na mume wangu, tulikuwa tunasali kwa Nabii Flora Peter, ambaye
baada ya kumweleza mazingira ya kifo hiki, alimuweka kwenye maombi na
kututaka tumpelekee picha yake,”
“Baada
ya maombi alitueleza kuwa anamuona mtoto wetu yupo hai na anaamini
atarudi siku moja. Tuliendelea na maombi na siku moja nilikutana na mama
Mariamu ambaye baada ya kumwelezea kifo cha mtoto wangu, aliniambia
kuna kijana anaitwa Bino ambaye anaweza kumrudisha kama alikufa
kichawi,”
Alisema mama huyo alimpa namba ya mtu huyo na alipowasiliana naye, Bino alimtaka ashike Sh. 100.
“Nilifanya
hivyo na baada ya dakika tano tukiwa bado hewani, alinijulisha kuwa
mtoto wangu anamuona yupo hai hivyo akanitaka niende kesho yake Dodoma
kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo ya kumrudisha,”
Hellena
alisema siku iliyofuata alisafiri kuelekea Dodoma na aliwasili saa
10:00 jioni ambapo alienda moja kwa moja kwa mganga huyo.
“Saa
1:00 jioni Bino alichukua mwiko, ungo na kinu, vifaa anavyovitumia
kwenye kazi yake. Ungo aliuweka chini na akaanza kusoma dua kisha
nikamuona mtoto amekaa ndani ya ungo ule, nilishtuka sana baada ya
kumwona akiwa hana hata nguo, amechafuka na aliyechoka,” alisema.
Alisema baada ya tukio hilo, mtoto alibaki kwa mganga huyo kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi.
Alisema alikaa kwa mganga huyo kwa muda wa siku mbili na kurudi Dar es Salaam na kumuacha mtoto huko kama alivyotakiwa.
“Jana
aliletwa na Bino ili aje kutusalimia kwa kweli nashukuru Mungu kwa
sababu hali ya mwanangu inaendelea vizuri, afya yake ipo vizuri, ”
alisema.
Baba
wa mtoto huyo, Joseph, alisema kuwa tukio hilo ni la kwanza na la aina
yake kwenye ukoo wao na kwamba lilipotokea hakuna aliyeamini hadi
walipomuona mtoto.
Alisema
baada ya mtoto wake kuletwa, majirani ambao walishiriki kwenye msiba
wake, walishtuka na kujaa nyumbani kwake kitendo ambacho kiliwalazimu
kwenda polisi kutoa taarifa ya kile kilichotokea.