Jumapili, 28 Desemba 2014

UVCCM MBEYA, KUWASHUKURU WAPIGA KURA


JUMUIYA ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Mbeya, imeandaa ziara ya kuwashukuru wananchi waliokipigia kura chama hicho katika uchaguzi wa serikali za Mitaa, uliofanyika Desemba 14, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna, alisema kuwa, katika ziara hiyo wataambatana na Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Sixtus Mapunda.
 
Alisema ziara hiyo wataianza January 5,2015 wilayani Mbarali na kuhiitimisha wilayani Momba Januari 9, 2015 ambapo pamoja na mambo mengine ya vikao vya ndani, Katibu Mkuu wao atahutubia mikutano ya hadhara.
“Kimsingi ziara hii ni ya Katibu Mkuu, ambaye ataifanya katika wilaya za Mbarali, Mbeya Mjini, Mbeya Vijijini, Mbozi na Momba. Wilaya zilizobaki za Ileje, Chunya, Rungwe na Kyela ratiba itatolewa baadae” alisema Kajuna.
Kwa upande wake Katibu wa UVCCM Mkoani hapa, Adia Mamu, alisema maandaliazi yanaendelea katika wilaya zote ambazo katibu Mkuu wa UVCCM Taifa atafanya vikao na kuhutubia mikutano ya hadhara na amewaomba wananchi kujitokeza kwa ajili ya kusikiliza mikutano hiyo.

 Wakati huo huo, kesho Desemba 29, mwaka huu, Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupitia umoja wa vijana wa chama hicho (BAVICHA), kinatarajia kufanya mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Mbalizi, wilaya ya Mbeya Vijijini kwa lengo la kuwashukuru wananchi baada ya Mwenyekiti wa mtaa huo, Elia Mkono(Chadema) kuchaguliwa.
                          
                            BY KALULUNGA  MEDIA 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni