Ijumaa, 21 Novemba 2014

UFISADI WA ESCROW WAZUA SOKOMOKO BUNGENI, KUMTAFUTA NANI MCHAWI.

 
  Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza bungeni Dodoma jana.


Dodoma. Kitimtim bungeni. Hicho ndicho kilichotokea bungeni jana baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuwaomba wabunge kukishauri kiti chake juu ya hatua ya kuwasilishwa na kujadiliwa kwa ripoti ya uchunguzi wa IPTL kwa madai ya kuwapo kesi mahakamani.
Wabunge wa pande zote – chama tawala na upinzani  waliopata fursa ya kuzungumza, walitoa kauli zinazofanana za kutaka suala hilo lijadiliwe na chombo hicho cha kutunga sheria, huku wakipinga njama za kutaka kuzima hoja.
Hata pale Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipojaribu kueleza umuhimu wa kumaliza suala hilo bila mihimili ya Bunge na Mahakama kuingiliana, zilisikika sauti wabunge wakimzomea, ikimaanisha kuwa suala hilo lazima lijadiliwe kwa uwazi bungeni.
Kwa jinsi mjadala huo wa wabunge ulivyokwenda, ni dhahiri kwamba ripoti hiyo iliyochunguza kuchotwa kwa Sh306 bilioni katika akaunti ya Tegeta Escrow italeta mtikisiko mkubwa serikalini na bungeni kama ambavyo gazeti hili liliripoti Jumanne iliyopita.
Wabunge wanane waliochangia mjadala huo walionekana wazi kutaka kiti cha Spika kitumie mamlaka yake vizuri kuhakikisha ripoti hiyo inawasilishwa bungeni haraka na kujadiliwa ili waliochota fedha hizo “wabebe msalaba wao”.
Mjadala huo mkali uliibuka baada ya kuibuka taarifa kwamba kuna barua kutoka mahakamani iliyowasilishwa kwa Bunge kutaka kuzuiwa kwa mjadala huo, barua ambayo hata hivyo, Ndugai alisema hajaiona.
Naibu Spika alitoa fursa hiyo baada ya kuombwa mwongozo na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila aliyetaka kujua iwapo ripoti hiyo itawasilishwa bungeni au la, kutokana na kuwapo kwa madai ya barua kutoka mahakamani.
“Tunataka tujue ripoti italetwa au la, tunasikia kuna mkakati wa kimahakama kuzuia isije, sasa tunataka utuhakikishie kama itaingia bungeni kwa kuwa Mahakama haipaswi kuingilia Bunge,” alisema Kafulila.
Kabla ya kujibu mwongozo huo, Ndugai alisema: “Kama mlivyozungumza hili ni jambo la haki za Bunge, sasa naomba mkisaidie kiti tujadili mwelekeo.”
Kafulila
Aliyepewa nafasi ya kufungua mjadala huo ni Kafulila aliyeanza kwa kutoa ushauri kwa kiti cha Spika kuwa Bunge ndilo lenye mamlaka ya mwisho na wabunge ndiyo wawakilishi wa wananchi, hivyo kuna mtihani kuhusu jambo hilo na Bunge ndilo litaamua.
“Ni lazima tujue kama Bunge tunatosha au hatutoshi, kama Bunge linaweza au haliwezi. Kama taarifa zinasema kuna majaji na viongozi wamekula fedha hizo halafu kuna hoja ya kuzuia eti jambo liko mahakamani. Hilo jambo halina msingi kama kweli kuna hoja ya Mahakama mbona CAG alipochunguza kwa niaba ya Bunge haikuzuia?”
Alisema ni lazima Bunge lifanye uamuzi kama ilivyoamuliwa tangu mwanzo.
Bulaya
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema lazima Bunge liheshimiwe kwa kuwa haiwezekani mhimili mmoja ukaingilia mwingine na kujifanya uko juu.
“Sisi tunachojadili hapa ni ripoti ya CAG na hii ni ripoti ya Bunge na si ya Serikali. Hatujadili kesi hizo alizosema Waziri Mkuu, hatuwezi kukubali Mahakama moja ikatoa uamuzi tofauti katika jambo moja,” alisema Bulaya.
Alisema ni muhimu Bunge likaendelea na ratiba yake kuhusu ripoti hiyo na kila mtu achukuliwe hatua kwa kile alichokitenda.
Lekule Laizer
Mbunge wa Longido (CCM), Michael Lekule Laizer alisema wabunge wengine hawalielewi suala la escrow lakini kama kweli kuna wezi ndani ya Bunge wachukuliwe hatua na ripoti hiyo iwasilishwe bungeni.
“Hili jambo ni kubwa na tumegawanyika kwa kuwa wengine hatulijui vizuri. Kama kuna wezi humu ndani au nje ya Bunge naomba Naibu Spika tusifiche maovu, tusifuge wezi, hivyo ripoti ije haraka na liwe ni jambo la dharura, waliokula wabainike na washughulikiwe.
“Hili jambo lijadiliwe na Kamati ya Uongozi ikae leo (jana) ili jambo hili lije kwenye ratiba ya kesho (leo),” alisema Laizer na kushangiliwa na wabunge wengi.
Msigwa
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema huu ndiyo muda wa kusema ukweli, hakuna kufunika kombe mwanaharamu apite... “safari hii mwanaharamu hapiti.
“Huu ni wakati mwafaka wa kujua tumbili ni nani na mwizi ni nani. Kama kuna majaji au maaskofu na mawaziri tunataka ijulikane. Mara nyingi Serikali inajaribu kufichaficha, lakini haiwezekani kufichaficha haya mambo sasa,” alisema Msigwa.


Msigwa alimchokonoa aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kwamba wakati huo, Dk Willibrod Slaa aliwahi kuwasilisha nyaraka za kashfa bungeni lakini (Sitta) akasema ni za intaneti hivyo hazina ukweli, lakini baadaye zikaonekana za kweli,  jambo ambalo Sitta alilijibu hapohapo akimwita Msigwa kuwa ni hasimu wake na kuwa kweli Dk Slaa aliwasilisha nyaraka hizo ambazo nyingine zilikuwa na madai ya ukweli na nyingine za uongo.
Lembeli
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli alisema  ni lazima kila mtu abebe msalaba wake kama ni wabunge wabebe msalaba wao, viongozi pia wabebe misalaba yao. Wakati Lembeli akizungumza hayo wabunge wengine walikuwa wakiitikia amen, amen, amen.
Lembeli alisema nchi inaweza kuingia kwenye machafuko au vurumai ikiwa taasisi ambayo wananchi wanaiamini haitawatendea haki. “Wananchi wanaamini taasisi mbili ambazo ni JWTZ na Bunge, sasa hiyo mikakati inayofanywa na taasisi nyingine haiaminiki kwa kuwa hata Mahakama haiaminiki,” alisema Lembeli.
Alisema fedha zimeliwa na watu ndani ya Bunge halafu yeye kama mbunge akawaambie wananchi wachangie maabara wakati fedha zilizochotwa zinaweza kujenga maabara zote nchini.
“Kama ni mtego utegue Naibu Spika, historia itakukumbuka kwa kuwa kuna wengine humu eti wamechukua Sh1 bilioni kwa consultant (ushauri) na mtu yupo humu,” alisema Lembeli.
Mbatia
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia alisema nchi inayumba kwa kuwa Serikali haiaminiki kitu ambacho ni hatari. “Kwa kuwa kuna tatizo tusiruhusu kulaumiwa na historia kutuhukumu. Kiti kitumie hekima na busara tumalizane na jambo hili ili nchi itulie.
“Tunahitaji uadilifu, uaminifu, hivyo tusikubali kuzima hili jambo. Naomba tuache miswada yote tumalizane na hili ili utulivu uwepo,” alisema Mbatia.
Lissu
Akizungumza kwa niaba ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema si kanuni za Bunge, Katiba wala sheria yoyote inayoruhusu Mahakama kuingilia shughuli za Bunge wala kumfundisha Spika namna ya kuendesha Bunge.
“Hakuna huo utaratibu wa kukufundisha wewe kuongoza Bunge, hivyo kama kuna barua imetoka mahakamani kwa jaji fulani naomba iwekwe mezani ili tumjadili huyo jaji, kama barua hiyo haipo basi tuendelee na shughuli zetu,” alisema Lissu ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani.
 
Aliongeza: “Leo Naibu Spika nafasi yako ni ya kihistoria. Bunge la Tisa linakumbukwa kutokana na kashfa ya Richmond, basi hili Bunge la 10 litakumbukwa kwa Escrow na unao msalaba mkubwa na hakuna Simon Mkirene wa kukusaidia kubeba msalaba huo, hivyo hakikisha Bunge hili na nafasi yako vinaheshimika.”
Zitto
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) inayochambua ripoti hiyo, Zitto Kabwe alisema kwa jinsi kamati yake ilivyofanyia kazi jambo hilo, halikupaswa kutokea katika nchi yenye udhibiti wa dola kama Tanzania.
Alisema jambo hilo lingeweza kutokea kwenye nchi kama DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), Somalia au Sierra Leone lakini si kwa nchi yenye udhibiti wa dola.
“Suala hili ndiyo mstari wa uvumilivu wa Watanzania, lazima sisi kama wawakilishi wa wananchi tujue nini cha kufanya.”
Alisema wakati jambo hili lilipoanza, yalisikika mengi ya kuzusha na minong’ono mingi na ili kuyamaliza yote hayo lazima lijadiliwe kwa uwazi bungeni, hivyo wabunge wajiandae kupambana na facts (ukweli) zitakazowekwa mezani badala ya kupambana na watu.”
Zitto alisema kamati yake iko tayari wakati wowote kuwasilisha ripoti hiyo bungeni kwani kazi yao imemalizwa na wakuu wa TRA, CAG na Takukuru baada ya kukutana nao.
Pinda
Baada ya wabunge hao kusema hayo, kama kukisaidia kiti cha Spika, Ndugai alitoa nafasi kwa Waziri Mkuu  Pinda kusema lolote na alisema mihimili mitatu ya nchi ipo kwa mujibu wa Katiba na kila chombo kipo kwa kanuni zake.
Alisema kauli ya kwamba Mahakama inatumika kama chombo cha kuficha uozo siyo kauli nzuri. “Ningependa sana jambo hili liishe ila tuangalie busara ili kila mhimili utekeleze jukumu lake kwa urahisi,” alisema Pinda kauli ambayo iliwafanya wabunge waanze kuzomea kwa kuonyesha kutokufurahishwa nayo.
Ndugai
Pinda alipomaliza, Ndugai alisema: “Mambo haya ni magumu sana kama alivyosema Waziri Mkuu. Kazi ya Jaji Mkuu ni kulinda mhimili wa Mahakama, tena kwa wivu kabisa na kazi ya Spika ni kulinda Bunge, tena kwa wivu kabisa.”

Baada ya kauli hiyo ambayo ilipokewa kwa shangwe na wabunge, alisema wakati Sitta alipokuwa Spika aliwahi kuwaambia katika Kamati ya Uongozi kuwa, ‘Tukiwa viongozi hatuwezi kutengeneza umoja katika maovu’ na kwamba kutokana na  kauli hiyo, Bunge haliwezi kuficha uovu katika jambo hilo na kwamba litashughulikiwa vizuri na haki itatendeka.
Kabla ya mjadala
Awali, katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Pinda alisema kuwa kuna kesi zaidi ya 10 kuhusu IPTL mahakamani, ambazo ni za wadau wanaohusiana na jambo hilo.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali aliyetaka kujua Serikali ina kauli  gani kuhusu taarifa ya kwamba Mahakama imeliandikia Bunge barua ili suala la Tegeta Escrow lisijadiliwe ili kuwanasua wale wanaohusika.
Pinda alisema kesi hizo ndani yake zinahusiana na fedha hizo hizo za escrow, hivyo kwa mfumo na msingi wa utawala wa sheria nchini, linapokuwapo jambo linaloendelea mahakamani, utaratibu wa kikatiba unawataka wao ambao ni upande wa mhimili mwingine kuacha kuanza kujadili jambo hilo kwa umma kwa sababu utaingilia kile kinachoendelea.
“Najaribu kueleza tu lakini haya ni maoni yangu, bado Ofisi ya Spika itaweza kupata ushauri mzuri na tutajua wanasema nini, kwa hiyo si mara ya kwanza mambo kama haya kuwapo na wote tumekuwa tukiheshimu kilichokuwa kinaendelea mahakamani,” alisema Pinda.
Akijibu swali la awali la Machali kuhusu kauli yake kwamba fedha hizo za escrow si za Serikali, Pinda alisema anajua suala hilo liko katika Ofisi ya Spika lakini angeeleza nini kilichotokea kwa uelewa wake.
Alisema msingi wake wa kusema hivyo ulitokana na uelewa wake kwamba Tanzania ilitumia umeme uliokuwa unazalishwa na Kampuni ya IPTL.
Pinda alisema katika maelewano ya awali ambayo yalikuwa yamekwishakubalika, alijua kwamba fedha zinazotolewa ni kwa sababu ya matumizi ya umeme nchini.
“Ndiyo maana nikasema kwa uelewa ambao ni msingi tu, fedha zile ni kwa ajili ya kwenda kulipa ankara za umeme tuliokuwa tumekwishatumia. Hata hivyo, kwa kuwa jambo hili liko chini ya uchunguzi wa Takukuru na CAG, hivyo uchunguzi utatuambia kama upande wa Serikali kipo kiasi cha fedha ambacho kilitakiwa tulipwe, naamini utaratibu huo utafuatwa, alisema Pinda.
“Kama itaonekana katika mchakato huo kuna upungufu umejitokeza na chunguzi hizo zikionyesha hivyo, Serikali haitasita kuchukua hatua zozote za kisheria. Takukuru akifanya uamuzi kwamba kwa Pinda kuna tatizo katika suala hili, hakuna mswalie mtume Pinda atakwenda tu.”

                                                        NA:- MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni