Jumanne, 25 Novemba 2014

Waandamanaji wafanya vurugu St.Louis

  Mji wa St Louis limeshuhudia maandamano na vitendo vya uporaji baada ya jaji kupitisha uamuzi wa kumshtaki aliyemuua kijana mweusi Michael Brown.
  Polisi mjini humo wamesema vurugu zimeleta madhara makubwa zaidi kuliko ya mwezi Agosti baada ya kuuawa kwa kijana huyo.
Kamanda wa Polisi wa St Louis, Jon Belmar amesema alisikia milio ya risasi takriban 150 kutoka kwenye makundi ya watu.
   Brown alifyatuliwa risasi na Polisi tarehe 9 Mwezi Agosti, hali iliyoibua ghadhabu na maandamano.
Watu wengi wa jamii ya Afrika na Marekani walitoa wito wakitaka     Afisa Polisi Darren Wilson ashtakiwe kwa mauaji.
Rais wa Marekani Barack Obama alitoa wito kwa wamarekani kuwa watulivu na kukubali maamuzi ya Jaji kuhusu kesi hiyo.

Jengo laanguka, Kumi wafa Misri

   Vikosi vya uokoaji vikitafuta Watu walionasa kwenye kifusi cha Jengo


  Watu kumi wamepoteza maisha baada ya jengo la ghorofa kuanguka mjini Cairo nchini Misri, maafisa wameeleza.
Watu saba wamejeruhiwa baada ya jengo la ghorofa nane kuanguka usiku.
Mkuu wa Idara ya dharula Jenerali Mamdouh Abdul Qader amesema vikosi vya uaokoaji vinawasaka Watu 15 wanaokisiwa kunasa kwenye kifusi.
Mara kadhaa majengo yameanguka nchini humo, sababu kubwa ikiwa ujenzi usiofuata kanuni na Sheria pia usimamizi mbovu wa taratibu za ujenzi.
Jenerali Qader ameliambia shirika la Habari la Ufaransa kuwa hawajui chanzo cha ajali hiyo,lakini walipatiwa taarifa kuwa ghorofa mbili za juu zilijengwa kinyume cha sheria.
Wakazi wa majengo ya karibu na lilipoanguka jengo hilo wameondoka katika makazi yao kwa nia ya kujihadhari.
Mwezi Januari Mwaka jana,Watu 28 walipoteza maisha baada ya jengo la ghorofa nane kuanguka mjini Alexandria.

Jumatatu, 24 Novemba 2014

Wavuvi 50 wauawa na Boko Haram

Taarifa kutoka Kaskazini Mashariki mwa Nigeria zinasema kuwa wanamgambo wa Boko Haram wamefanya shambulizi lengine kubwa sana na kuwaua takriban wafanya biashara 50 wa kuuza Samaki katika ufuo wa ziwa Chad.
Shambulio hilo lilifanyika Alhamisi lakini kutokana na matatizo ya kimitambo, taarifa za mauaji hayo hazikuweza kutolewa punde yalipofanyika.
Siku moja kabla ya mauaji hayo, zaidi ya watu arobaini waliuwa na wanamgambo hao, katika shambulizi lililofanya peupe mchana katika jimbo la Borno.
Wafanyabiashara hao, walikuwa njiani kununua Samaki waliposhambuliwa na wapiganaji wa Boko Haram.
Boko Haram waliziba barabara karibu na kijiji cha Doron Baga na kulingana na kiongozi mkuu wa shirika la wafanyakazi hao wakawachinja wengi wa waathiriwa wengine wakifungwa kamba na kuzamishwa majini katika ziwa Chad


Maelfu ya watu wameachwa bila makao kufuatia harakati za kundi hilo Kaskazini Mashariki mwa Nigeria
Nia ya shambulizi lao haikujulikana mara moja.Eneo lililoshambuliwa linapaswa kuwa na kikosi cha wanajeshi kinachoshika doria, lakini kikosi cha wanajeshi hao kutoka Nigeria , Chad na Niger hakijaweza kudhibiti hali katika eneo lenyewe kama ilivyotarajiwa kwani wameshindwa kulikomesha kundi la Boko Haram kufanya mashambulizi ya mara kwa mara.
Hili lilikuwa shambulizi la pili kubwa kufanyika katika jimbo la Borno wiki jana na kwa jumla takriban watu 100 waliuawa.
Mnamo siku ya Jumatano, wapiganaji hao walivamia soko moja katika eneo la Aazara Kuya. Watu 45 walikamatwa huku wakifungwa mikono na kukatwa koo zao.
Shambulizi hili inaarifiwa lililengwa kuadhibu jamii baada ya wanamgambo wanne kutambulishwa kwa wanajeshi na kuuawa.

Upinzani Nigeria walaani uvamizi

Uchaguzi utafanyika mwezi Februari nchini Nigeria


  Chama cha upinzani nchini Nigeria, kimelaani uvamizi uliofanywa na maafisa wa usalama dhidi ya ofisi zake mjini Lagos mwishoni mwa wiki.
"Tunataka uchunguzi huru ufanywekubaini sababu zilizopelekea maafisa waliokuwa wamejihami kuvamia ofisi zetu, '' alisema naibu mwenyekiti wa chama cha upinzani cha (APC) Lawal Shuaibu t
Chama hicho kilisema ,komputa zake pamoja na nyaraka nyinginezo ziliporwa wakati wa msako huo.

Wakuu wa usalama wanasema wanachunguza madai ya chama hicho kutengeza kadi bandia za wapiga kura kabla ya uchaguzi kufanyika mwezi Februari.

Maafisa wa usalama walidai kuwa chama hicho kilikuwa kinatengeza kadi bandia kwa lengo la kuvamia mtandao wa tume ya uchaguzi kwa lengo la kubadilisha data ya tume hiyo.
Kwa sasa maafisa wa usalama wameweka vifaa vya udukuzi kwa ofisi hio baada ya kuhakikisha kuwa baadhi ya shughuli zinazoendelea katika jengo hilo, zinakwenda kinyume na sheria.

Chama hicho kimesema kuwa maafisa wa usalama walitwaa nyaraka, tarakilishi na vifaa vingine vya kielektroniki.

Ijumaa, 21 Novemba 2014

UFISADI WA ESCROW WAZUA SOKOMOKO BUNGENI, KUMTAFUTA NANI MCHAWI.

 
  Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza bungeni Dodoma jana.


Dodoma. Kitimtim bungeni. Hicho ndicho kilichotokea bungeni jana baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuwaomba wabunge kukishauri kiti chake juu ya hatua ya kuwasilishwa na kujadiliwa kwa ripoti ya uchunguzi wa IPTL kwa madai ya kuwapo kesi mahakamani.
Wabunge wa pande zote – chama tawala na upinzani  waliopata fursa ya kuzungumza, walitoa kauli zinazofanana za kutaka suala hilo lijadiliwe na chombo hicho cha kutunga sheria, huku wakipinga njama za kutaka kuzima hoja.
Hata pale Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipojaribu kueleza umuhimu wa kumaliza suala hilo bila mihimili ya Bunge na Mahakama kuingiliana, zilisikika sauti wabunge wakimzomea, ikimaanisha kuwa suala hilo lazima lijadiliwe kwa uwazi bungeni.
Kwa jinsi mjadala huo wa wabunge ulivyokwenda, ni dhahiri kwamba ripoti hiyo iliyochunguza kuchotwa kwa Sh306 bilioni katika akaunti ya Tegeta Escrow italeta mtikisiko mkubwa serikalini na bungeni kama ambavyo gazeti hili liliripoti Jumanne iliyopita.
Wabunge wanane waliochangia mjadala huo walionekana wazi kutaka kiti cha Spika kitumie mamlaka yake vizuri kuhakikisha ripoti hiyo inawasilishwa bungeni haraka na kujadiliwa ili waliochota fedha hizo “wabebe msalaba wao”.
Mjadala huo mkali uliibuka baada ya kuibuka taarifa kwamba kuna barua kutoka mahakamani iliyowasilishwa kwa Bunge kutaka kuzuiwa kwa mjadala huo, barua ambayo hata hivyo, Ndugai alisema hajaiona.
Naibu Spika alitoa fursa hiyo baada ya kuombwa mwongozo na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila aliyetaka kujua iwapo ripoti hiyo itawasilishwa bungeni au la, kutokana na kuwapo kwa madai ya barua kutoka mahakamani.
“Tunataka tujue ripoti italetwa au la, tunasikia kuna mkakati wa kimahakama kuzuia isije, sasa tunataka utuhakikishie kama itaingia bungeni kwa kuwa Mahakama haipaswi kuingilia Bunge,” alisema Kafulila.
Kabla ya kujibu mwongozo huo, Ndugai alisema: “Kama mlivyozungumza hili ni jambo la haki za Bunge, sasa naomba mkisaidie kiti tujadili mwelekeo.”
Kafulila
Aliyepewa nafasi ya kufungua mjadala huo ni Kafulila aliyeanza kwa kutoa ushauri kwa kiti cha Spika kuwa Bunge ndilo lenye mamlaka ya mwisho na wabunge ndiyo wawakilishi wa wananchi, hivyo kuna mtihani kuhusu jambo hilo na Bunge ndilo litaamua.
“Ni lazima tujue kama Bunge tunatosha au hatutoshi, kama Bunge linaweza au haliwezi. Kama taarifa zinasema kuna majaji na viongozi wamekula fedha hizo halafu kuna hoja ya kuzuia eti jambo liko mahakamani. Hilo jambo halina msingi kama kweli kuna hoja ya Mahakama mbona CAG alipochunguza kwa niaba ya Bunge haikuzuia?”
Alisema ni lazima Bunge lifanye uamuzi kama ilivyoamuliwa tangu mwanzo.
Bulaya
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema lazima Bunge liheshimiwe kwa kuwa haiwezekani mhimili mmoja ukaingilia mwingine na kujifanya uko juu.
“Sisi tunachojadili hapa ni ripoti ya CAG na hii ni ripoti ya Bunge na si ya Serikali. Hatujadili kesi hizo alizosema Waziri Mkuu, hatuwezi kukubali Mahakama moja ikatoa uamuzi tofauti katika jambo moja,” alisema Bulaya.
Alisema ni muhimu Bunge likaendelea na ratiba yake kuhusu ripoti hiyo na kila mtu achukuliwe hatua kwa kile alichokitenda.
Lekule Laizer
Mbunge wa Longido (CCM), Michael Lekule Laizer alisema wabunge wengine hawalielewi suala la escrow lakini kama kweli kuna wezi ndani ya Bunge wachukuliwe hatua na ripoti hiyo iwasilishwe bungeni.
“Hili jambo ni kubwa na tumegawanyika kwa kuwa wengine hatulijui vizuri. Kama kuna wezi humu ndani au nje ya Bunge naomba Naibu Spika tusifiche maovu, tusifuge wezi, hivyo ripoti ije haraka na liwe ni jambo la dharura, waliokula wabainike na washughulikiwe.
“Hili jambo lijadiliwe na Kamati ya Uongozi ikae leo (jana) ili jambo hili lije kwenye ratiba ya kesho (leo),” alisema Laizer na kushangiliwa na wabunge wengi.
Msigwa
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema huu ndiyo muda wa kusema ukweli, hakuna kufunika kombe mwanaharamu apite... “safari hii mwanaharamu hapiti.
“Huu ni wakati mwafaka wa kujua tumbili ni nani na mwizi ni nani. Kama kuna majaji au maaskofu na mawaziri tunataka ijulikane. Mara nyingi Serikali inajaribu kufichaficha, lakini haiwezekani kufichaficha haya mambo sasa,” alisema Msigwa.


Msigwa alimchokonoa aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kwamba wakati huo, Dk Willibrod Slaa aliwahi kuwasilisha nyaraka za kashfa bungeni lakini (Sitta) akasema ni za intaneti hivyo hazina ukweli, lakini baadaye zikaonekana za kweli,  jambo ambalo Sitta alilijibu hapohapo akimwita Msigwa kuwa ni hasimu wake na kuwa kweli Dk Slaa aliwasilisha nyaraka hizo ambazo nyingine zilikuwa na madai ya ukweli na nyingine za uongo.
Lembeli
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli alisema  ni lazima kila mtu abebe msalaba wake kama ni wabunge wabebe msalaba wao, viongozi pia wabebe misalaba yao. Wakati Lembeli akizungumza hayo wabunge wengine walikuwa wakiitikia amen, amen, amen.
Lembeli alisema nchi inaweza kuingia kwenye machafuko au vurumai ikiwa taasisi ambayo wananchi wanaiamini haitawatendea haki. “Wananchi wanaamini taasisi mbili ambazo ni JWTZ na Bunge, sasa hiyo mikakati inayofanywa na taasisi nyingine haiaminiki kwa kuwa hata Mahakama haiaminiki,” alisema Lembeli.
Alisema fedha zimeliwa na watu ndani ya Bunge halafu yeye kama mbunge akawaambie wananchi wachangie maabara wakati fedha zilizochotwa zinaweza kujenga maabara zote nchini.
“Kama ni mtego utegue Naibu Spika, historia itakukumbuka kwa kuwa kuna wengine humu eti wamechukua Sh1 bilioni kwa consultant (ushauri) na mtu yupo humu,” alisema Lembeli.
Mbatia
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia alisema nchi inayumba kwa kuwa Serikali haiaminiki kitu ambacho ni hatari. “Kwa kuwa kuna tatizo tusiruhusu kulaumiwa na historia kutuhukumu. Kiti kitumie hekima na busara tumalizane na jambo hili ili nchi itulie.
“Tunahitaji uadilifu, uaminifu, hivyo tusikubali kuzima hili jambo. Naomba tuache miswada yote tumalizane na hili ili utulivu uwepo,” alisema Mbatia.
Lissu
Akizungumza kwa niaba ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema si kanuni za Bunge, Katiba wala sheria yoyote inayoruhusu Mahakama kuingilia shughuli za Bunge wala kumfundisha Spika namna ya kuendesha Bunge.
“Hakuna huo utaratibu wa kukufundisha wewe kuongoza Bunge, hivyo kama kuna barua imetoka mahakamani kwa jaji fulani naomba iwekwe mezani ili tumjadili huyo jaji, kama barua hiyo haipo basi tuendelee na shughuli zetu,” alisema Lissu ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani.
 
Aliongeza: “Leo Naibu Spika nafasi yako ni ya kihistoria. Bunge la Tisa linakumbukwa kutokana na kashfa ya Richmond, basi hili Bunge la 10 litakumbukwa kwa Escrow na unao msalaba mkubwa na hakuna Simon Mkirene wa kukusaidia kubeba msalaba huo, hivyo hakikisha Bunge hili na nafasi yako vinaheshimika.”
Zitto
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) inayochambua ripoti hiyo, Zitto Kabwe alisema kwa jinsi kamati yake ilivyofanyia kazi jambo hilo, halikupaswa kutokea katika nchi yenye udhibiti wa dola kama Tanzania.
Alisema jambo hilo lingeweza kutokea kwenye nchi kama DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), Somalia au Sierra Leone lakini si kwa nchi yenye udhibiti wa dola.
“Suala hili ndiyo mstari wa uvumilivu wa Watanzania, lazima sisi kama wawakilishi wa wananchi tujue nini cha kufanya.”
Alisema wakati jambo hili lilipoanza, yalisikika mengi ya kuzusha na minong’ono mingi na ili kuyamaliza yote hayo lazima lijadiliwe kwa uwazi bungeni, hivyo wabunge wajiandae kupambana na facts (ukweli) zitakazowekwa mezani badala ya kupambana na watu.”
Zitto alisema kamati yake iko tayari wakati wowote kuwasilisha ripoti hiyo bungeni kwani kazi yao imemalizwa na wakuu wa TRA, CAG na Takukuru baada ya kukutana nao.
Pinda
Baada ya wabunge hao kusema hayo, kama kukisaidia kiti cha Spika, Ndugai alitoa nafasi kwa Waziri Mkuu  Pinda kusema lolote na alisema mihimili mitatu ya nchi ipo kwa mujibu wa Katiba na kila chombo kipo kwa kanuni zake.
Alisema kauli ya kwamba Mahakama inatumika kama chombo cha kuficha uozo siyo kauli nzuri. “Ningependa sana jambo hili liishe ila tuangalie busara ili kila mhimili utekeleze jukumu lake kwa urahisi,” alisema Pinda kauli ambayo iliwafanya wabunge waanze kuzomea kwa kuonyesha kutokufurahishwa nayo.
Ndugai
Pinda alipomaliza, Ndugai alisema: “Mambo haya ni magumu sana kama alivyosema Waziri Mkuu. Kazi ya Jaji Mkuu ni kulinda mhimili wa Mahakama, tena kwa wivu kabisa na kazi ya Spika ni kulinda Bunge, tena kwa wivu kabisa.”

Baada ya kauli hiyo ambayo ilipokewa kwa shangwe na wabunge, alisema wakati Sitta alipokuwa Spika aliwahi kuwaambia katika Kamati ya Uongozi kuwa, ‘Tukiwa viongozi hatuwezi kutengeneza umoja katika maovu’ na kwamba kutokana na  kauli hiyo, Bunge haliwezi kuficha uovu katika jambo hilo na kwamba litashughulikiwa vizuri na haki itatendeka.
Kabla ya mjadala
Awali, katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Pinda alisema kuwa kuna kesi zaidi ya 10 kuhusu IPTL mahakamani, ambazo ni za wadau wanaohusiana na jambo hilo.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali aliyetaka kujua Serikali ina kauli  gani kuhusu taarifa ya kwamba Mahakama imeliandikia Bunge barua ili suala la Tegeta Escrow lisijadiliwe ili kuwanasua wale wanaohusika.
Pinda alisema kesi hizo ndani yake zinahusiana na fedha hizo hizo za escrow, hivyo kwa mfumo na msingi wa utawala wa sheria nchini, linapokuwapo jambo linaloendelea mahakamani, utaratibu wa kikatiba unawataka wao ambao ni upande wa mhimili mwingine kuacha kuanza kujadili jambo hilo kwa umma kwa sababu utaingilia kile kinachoendelea.
“Najaribu kueleza tu lakini haya ni maoni yangu, bado Ofisi ya Spika itaweza kupata ushauri mzuri na tutajua wanasema nini, kwa hiyo si mara ya kwanza mambo kama haya kuwapo na wote tumekuwa tukiheshimu kilichokuwa kinaendelea mahakamani,” alisema Pinda.
Akijibu swali la awali la Machali kuhusu kauli yake kwamba fedha hizo za escrow si za Serikali, Pinda alisema anajua suala hilo liko katika Ofisi ya Spika lakini angeeleza nini kilichotokea kwa uelewa wake.
Alisema msingi wake wa kusema hivyo ulitokana na uelewa wake kwamba Tanzania ilitumia umeme uliokuwa unazalishwa na Kampuni ya IPTL.
Pinda alisema katika maelewano ya awali ambayo yalikuwa yamekwishakubalika, alijua kwamba fedha zinazotolewa ni kwa sababu ya matumizi ya umeme nchini.
“Ndiyo maana nikasema kwa uelewa ambao ni msingi tu, fedha zile ni kwa ajili ya kwenda kulipa ankara za umeme tuliokuwa tumekwishatumia. Hata hivyo, kwa kuwa jambo hili liko chini ya uchunguzi wa Takukuru na CAG, hivyo uchunguzi utatuambia kama upande wa Serikali kipo kiasi cha fedha ambacho kilitakiwa tulipwe, naamini utaratibu huo utafuatwa, alisema Pinda.
“Kama itaonekana katika mchakato huo kuna upungufu umejitokeza na chunguzi hizo zikionyesha hivyo, Serikali haitasita kuchukua hatua zozote za kisheria. Takukuru akifanya uamuzi kwamba kwa Pinda kuna tatizo katika suala hili, hakuna mswalie mtume Pinda atakwenda tu.”

                                                        NA:- MWANANCHI

Jumatano, 19 Novemba 2014

Obama kutangaza mabadiliko ya uhamiaji

Ikulu ya Marekani imesema Rais Obama atatumia muda ambao watazamaji wa televisheni nchini humo wanaangalia zaidi  

           matangazo siku ya Alhamisi kutangaza mabadiliko makubwa ya mfumo wa uhamiaji wa nchi hiyo.
Inatarajiwa kuwa Rais Obama atasema kuwa atatumia madaraka yake aliyopewa kikatiba kuzuia wahamiaji wapatao milioni tano kurejeshwa makwao na badala yake wapatiwe vibali vya kufanya kazi nchini humo.

Rais Obama amesema hayo katika video iliyotumwa katika ukurasa wa facebook kabla ya hotuba yake.Tangu kuingia madaraka Obama amekuwa akipigania baadhi ya mabadiliko ikiwemo huduma ya utoaji wa huduma za afya kwa mfumo wa bima ya afya.

Jumanne, 18 Novemba 2014

Vijana wawaua 4 mjini Mombasa Kenya

Vijana mjini Mombasa
Watu wanne wameuawa kwa kudungwa visu na vijana waliokuwa wamejihami mjini Mombasa Pwani ya Kenya.
Watu kadhaa pia walijeruhiwa katika shambulio hilo la usiku wa kuamkia leo kwenye vituo vya basi Kisauni.
Mwandishi wa BBC mjini humo Emmanuel Igunza anasema hali ya wasiwasi imetanda Mombasa huku maafisa wa polisi wakipiga doria mitaani.
Walioshuhudia mashambulio hayo wanasema vijana waliokuwa wamejihami kwa mapanga na silaha nyingine butu, waliwavamia watu katika vituo vya magari ya abiria.
Aidha inadaiwa vijana hao walikuwa wameziba nyuso zao, wakipeperusha bendera nyeusi sawa na ile iliyopatikana katika msako wa jana kwenye miskiti ya Musa na Sakinah, jijini Mombasa.
Awali Polisi walionya kuwa wako tayari kukabiliana na chochote kitakachotokea kufuatia msako huo.
Zaidi ya vijana mia mbili hamsini walikamatwa na silaha kadhaa ikiwemo magurunedi na bastola kupatikana katika misikiti hiyo.
Hata hivyo viongozi wa Kiislamu na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu wamelaani msako huo, ambao wanasema utaenndeleza dhana kuwa polisi wanailenga jamii nzima ya waislamu.
Mwezi Februari, msako sawa na huo uliotekelezwa katika msikiti wa Musa ulisababisha ghasia na kifo cha afisa mmoja wa Polisi.

DRC:Polisi waliwaua vijana kiholela

Polisi wakipambana na vijana DRC
           
Ripoti ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu Human Rights Watch inasema polisi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa jumla wamewaua vijana wapatao 51 katika operesheni ya kupambana na uhalifu Kinshasa.
Watu wengine 33 hawajulikani waliko tangu operesheni hiyo ilopewa jina "Operation Likofi", ilioidhinishwa Kinshasa mwaka uliopita kufanyika.
Human Rights Watch liliwahoji zaidi ya maafisa 100 wa polisi, watu walioshuhudia nauaji hayo pamoja na jamaa wa waathiriwa.
     Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, liliwahoji zaidi ya maafisa 100 wa polisi , walioshuhudia matukio pamoja na jamaa wa waathiriwa waliotoa taarifa ya kile kilichosemekana kuwa mauaji ya kiholela.
    Msemaji wa shirika la hilo,(Anneke Van Woudenberg), alituhumu serikali kwa kuficha taarifa kuhusu mauaji hayo na kusema familia za waathiriwa zilikuwa zimetishwa na kuonywa dhidi ya kufichua taarifa za mauaji hayo.
     Ripoti iliyotolewa na umoja wa Mataifa mwaka jana pia ilielezea kuhusu mauaji hayo

Jumamosi, 1 Novemba 2014

MHE. PROFESA MARK MWANDOSYA AFUNGUKA, MBIO ZA URAIS 2015


ALIKIONGEA NA WAANDISHI WA HABARI JIJINI MBEYA KATIKA
 OFISI ZA CCM MKOA




BAADA ya kukaa kimya kwa muda mrefu kuzungumzia mbio za urais katika uchaguzi wa Mwakani, Hatimaye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Profesa Mark Mwandosya, ameibuka na kutoa duku duku lake.
Profesa Mwandosya  amewataka Wananchi kuwakataa wanaotumia fedha nyingi kulazimisha kuchaguliwa kuwa viongozi wao na badala yake wao ndiyo wawapendekeze.
         
Alisema anashangazwa sana na baadhi ya Wanachama kutumia fedha nyingi kulazimisha kupendekezwa ili agombee uongozi ndani ya Chama na Taifa jambo ambalo alisema ni kinyume na utaratibu ambao waliuacha waasisi wa Taifa na Chama.
Alisema ndani ya Chama kuna vitu vingi vinavyoangaliwa ikiwa ni pamoja na kumteua mtu atakayegombea Urais lakini wakati huo huo atakuwa Mwenyekiti wa Chama Taifa jambo ambalo wengi wao hawalitambui wanachojali ni kupata Urais pekee.
Alisema endapo wanachama wenzie watalitambua hilo litasaidia kuepusha mlolongo mkubwa ndani ya chama kwa kumteua mtu ambaye ataweza kudumisha fikra za Waasisi ikiwa ni pamoja na kuepuka migogoro isiyokuwa na faida yoyote kwa Wananchi.
Aliongeza kuwa Wananchi wanawajua watu wao ndani ya jamii  na kulinganisha na mfumo wa  ugomvi wa vijiji zamani ambapo Wananchi walikuwa wanamteua mtu ambaye ataweza kuongoza vita ya kukimbia kijiji kutokana na mapigano yanayokuwa yanaendelea.
Aliongeza kuwa mfumo wa sasa ni tofauti na mfumo iliokuwepo awali na mbao uliwekwa na waasisi pamoja na misingi ya vyama vya siasa ambapo hivi sasa kuna mtindo na imani kwamba fedha ndiyo msingi wa uteuzi na kuchaguliwa.
Alisema Watu wanatumia fedha vibaya kwa kuwanunua wajumbe, na kuwapa thamani wajumbe kwamba  mjumbe wa Mkutano mkuu thamani yake ni laki mbili, Mjumbe wa Nec Laki tano na Mjumbe wa Kamati Kuu thamani yake Milioni Moja.
Alisema hilo jambo Wananchi wanapaswa kulikataa kabisa na kama litaruhusiwa ikubalike kwamba maana ya siasa ni ya wenye fedha, sio ya wakulima na wafanya kazi, uongozi wa watu wenye fedha au mawakala waliowekwa na wenye fedha.
Aliongeza kuwa hiyo sio jadi iliyoachwa na Mwalimu Nyerere hivyo amewashauri wenye fedha nyingi kuzielekeza fedha hizo kwa wananchi kwa kuendeleza miundombinu ya afya, Elimu, maji na mahitaji ya jamii.
Aidha Profesa Mwandosya alijitolea mfano yeye mwenyewe kwamba hata ukijumlishwa mshahara wake tangu akiwa Waziri pamoja na safari za nje anazokwenda lakini bado hana uwezo wa kuhonga wajumbe wampitishe ili agombee urais.
Mwisho.

Na Mbeya yetu