Alhamisi, 24 Oktoba 2013

Uswisi sasa kurejesha mabilioni ya mafisadi

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (katikati) akiwa na maafisa wa Serikali ya Uswis pamoja na timu uchunguzi kufuatilia mabilioni ya fedha zilizowekwa katika benki za nchi hiyo. 

Picha na Bernhard Reinhold.

  ........................................................................

Dar es Salaam. Sakata la vigogo kuficha mabilioni ya shilingi katika benki za Uswisi, limechukua sura mpya baada ya Serikali ya nchi hiyo kutunga sheria inayowabana walioweka fedha kwenye benki zake kuzithibitisha, la sivyo zitarejeshwa katika nchi husika.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alifanya mazungumzo na Serikali ya nchi hiyo ambayo imemweleza kuwa imebadili sheria zake ili kuwadhibiti wageni wanaoficha fedha nchini humo.

Akizungumza na gazeti hili, Zitto alisema amepata taarifa hizo juzi baada ya kukutana na Waziri wa Fedha wa nchi hiyo ambaye alimwandalia mazungumzo na watalaamu wake.

Alibainisha kuwa tangu kuibuka kwa sakata hilo mwaka 2012 na Bunge kuiagiza Serikali kufuatilia, Serikali haijaomba taarifa yeyote kutoka Uswisi kuhusu Watanzania waliohifadhi fedha nchini humo.

“Jana nilikutana na Waziri wa Fedha na akatuacha na mazungumzo na wataalamu wake. Wamesema hadi sasa, Tanzania haijasaini mkataba wa kubadilishana taarifa za kikodi (Multilateral convention on administrative assistance in tax matters),” alisema Zitto na kuongeza;

“Kwa kutosaini, Tanzania inajinyima haki ya kupata taarifa hizi na kutoza kodi kwa watu walioficha fedha huku (Uswisi), maana Sheria ya Kodi ya Tanzania inataka kila Mtanzania popote anapopata kipato halali lazima alipe kodi.”

Zitto alieleza kuwa kitendo cha Serikali ya Uswisi kubadili sheria zake, kinaiwezesha nchi hiyo kutoa taarifa za benki za watu walioweka fedha nchini humo wakiwamo Watanzania, ambao sasa watatakiwa kuthibitisha kama fedha hizo ni safi au la.

“Kiufupi, Tanzania haijaomba taarifa yeyote kutoka Uswisi. Ila Uswisi wamebadili sheria yao na sasa mmiliki wa fedha ndiyo anapaswa kuthibitisha kwamba ni safi, na ikithibitika kuwa hazina mwenyewe wala maelezo, zitarudishwa nchi husika,” alisema.

Zitto alisema mbali na kukutana na watendaji hao wa Serikali amezungumza na Umoja wa Mabenki wa nchi hiyo uliobainisha kuwa Uswisi ina Watanzania wachache wenye fedha.

“Wamesema Watanzania wengi wana fedha Uingereza, Jersey, Cayman Islands na Mauritius. Dubai pia imetajwa sana,” alisema Zitto. Zitto alielezea kuwa umoja huo wa benki za Uswisi umeanzisha mkakati wa kusafisha fedha uitwao ‘clean money strategy’, na wamegundua watu wengi ambao ni wanasiasa, wamezuia akaunti zao na kupeleka majina kwenye Serikali zao.

“Tanzania haijafanya maombi rasmi hapa Uswisi na hivyo wao kama benki hawawezi tu kutoa taarifa bila kuombwa. Sheria yao imerekebishwa ambapo sasa ni wajibu wa mwenye akaunti kusema kama fedha zake ni halali au hapana,” alisema Zitto na kuongeza.

Hivi sasa hawapokei pesa kutoka nchi za Afrika au wanapokea kwa tahadhari sana, maana kuna reputational risk (kupoteza heshima),” alisema.

1 | 2 | 3 Next Page»

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni