Jumamosi, 27 Juni 2015

David Kafulila Amwandikia Barua Spika kudai ripoti ya mabehewa Feki


MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), amemuandikia barua Spika wa Bunge, Anne Makinda, kudai aielekeze Serikali kuleta ripoti ya uchunguzi wa tuhuma za ununuzi  wa mabehewa kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Kafulila alisema mbali na barua hiyo, pia ataendelea kulizungumzia suala hilo bungeni hadi ripoti hiyo itakapoletwa bungeni.

Alisema jambo hilo ni nyeti kwa kuzingatia kuwa taarifa ya awali ya Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA), ilibainisha wazi kuwa ununuzi wa mabehewa hayo uliofanywa na Kampuni ya Hidustan ya India ulikuwa na mapungufu.

“Mapungufu hayo ni pamoja na mabehewa kutozingatia viwango vilivyohitajika, kwa maana kulikuwa na udhaifu katika ‘Specifications’ na utangazaji zabuni ya mabehewa hayo. Wizara ya Uchukuzi haikuhakikisha uchunguzi wa uwezo na rekodi za kampuni kabla ya kupewa zabuni hiyo.

“Wizara ya Fedha ilifanya malipo mapema kinyume cha taratibu kabla ya mabehewa kufikishwa nchini,” alisema Kafulila.

Alisema Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta, alikiri kwamba alishapokea ripoti hiyo, hivyo haoni sababu ya kutokuletwa kwa taarifa ya utekelezaji  wake bungeni ili ijadiliwe na wabunge.

Alisema jambo hilo ni kubwa na linahusu uhai na gharama ya Sh bilioni 238.

Wakati Sitta akijibu hoja za wabunge wakati wa bajeti ya Wizara yake alisema watu watano wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kutokana na ufisadi huo.

Alisema kamati ya uchunguzi katika taarifa yake ilibaini kuwepo kwa makosa ya uzembe, hali iliyosababisha hasara ya Sh bilioni 12 na si Sh bilioni 238 kama inavyodaiwa.

Kamati iliyoundwa kuchunguza sakata hilo  iliihusisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mwanasheria Mkuu (AG), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na wahandisi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni