Mbowe Azungumzia Kasi ya Rais Magufuli.....Adai Kuwa Mpinzani Haimaanishi Upinge Kila Kitu
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amezungumzia kasi aliyoanza nayo rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli pamoja na baraza lake la mawaziri.
Akizungumza
jana na mwandishi wa habari wa Azam TV, Mbowe alisema kuwa rais
Magufuli ameanza vizuri kiutendaji na kwamba ameanza kuzifanyia kazi
hoja zilizokuwa zikihubiriwa na Chadema ndani na nje ya Bunge.
“Hoja
ya kubana matumizi ya serikali, hoja ya kupunguza sherehe za kitaifa,
hoja ya kupunguza safari za nchi za nje kwa viongozi wetu, hoja ya
kupunguza watumishi wa umma ambao hawana umuhimu, hoja ya kuwa na
serikali ndogo. Haya mambo tulizungumza siku zote na hawa hawa wa Chama
cha Mapinduzi ndio waliokuwa wanayapinga haya,” alisema Mbowe.
Mbowe
alieleza kuwa dhana ya upinzani sio kupinga kila kitu kinachofanywa na
serikali hivyo chama chake hakitakuwa tayari kupinga mambo mema
yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano kama baadhi ya watu
wanavyotarajia, bali kitajikita katika kujadili na kuibua hoja za
msingi.
“Kuwa
mpinzani sio kupinga kila jambo linalofanyika hata kama likiwa jema.
Sasa sisi kama kambi rasmi ya upinzani bungeni na hata nje ya bunge ni
wajibu wetu katika wakati wote ule kuhakikisha tunaisimamia serikali ili
anachokisema rais kweli kitekelezwe kwa vitendo na isiwe hoja ya rais
pekee,”alisema.
Hata
hivyo, Mbowe alikosoa uteuzi wa baadhi ya mawaziri katika baraza la
serikali ya awamu ya tano hususan Dk. Harison Mwakyembe ambaye wizara ya
Uchukuzi aliyokua akiiongoza awali imekumbwa na sakata la upotevu wa
makontena bandarini na Profesa Sospeter Muhongo ambaye amerudishwa
katika wizara ya Nishati na Madini baada ya kujiuzulu katika nafasi hiyo
wakati wa serikali ya awamu ya nne kufuatia sakata la Escrow.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni