CAG Akaidi Agizo la Rais Magufuli....... Aenda Nairobi, Kenya Kwa Fedha za Serikali Bila Kibali Cha Ikulu
MDHIBITI
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad,
amekiuka agizo la Rais Dk. John Magufuli, baada kusafiri nje ya nchi
bila kibali cha Ikulu.
Kwa
mujibu wa gazeti la Mtanzania, CAG aliondoka nchini Jumamosi (Desemba
12, 2015) kwenda jijini Nairobi, Kenya na kurejea nchini Jumanne wiki
hii.
Taarifa
hizo, zimesema CAG alikwenda kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha
Nairobi, kazi ambayo haina uhusiano na ofisi yake, lakini alilipiwa
gharama zote na ofisi yake.
“Bosi
wetu aliondoka kwenda Nairobi Jumamosi iliyopita na kurejea Jumanne,
alikwenda kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Nairobi bila kibali cha
Ikulu, alipaswa kupata kibali kwa sababu ofisi yake ndio ililipa gharama
zote.
“Jumla ya gharama zinafika Sh milioni 15, ambazo ni pamoja na posho, tiketi ya ndege, hoteli na gharama nyinginezo,” kilisema chanzo cha gazeti hilo.
Alipoulizwa
kwa njia ya simu kuhusu safari hiyo, Profesa Assad hakuthibitisha wala
kukanusha taarifa hizo, zaidi ya kutishia kwenda mahakamani.
“Wewe
si umesema umepata taarifa kutoka vyanzo vyako na umenipigia ‘for
validation’, sasa mimi nakwambia hizo taarifa si za kweli na mkiandika
tutachukua hatua,” alijibu CAG.
Baada
ya muda, Profesa Assad alipiga simu kwa mhariri akimtaka afike ofisini
kwake akachukue nyaraka za kuthibitisha kuruhusiwa na kusafiri nje ya
nchi na ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Kutokana
na mhariri huyo kuwa nje ya Dar es Salaam, alimtuma mwandishi mwingine
kwenda katika ofisi ya CAG ili kuchukua nyaraka hizo. Mwandishi
alipofika, CAG alikataa kumpa wala kumwonesha nyaraka hizo.
Juhudi
za kumpata Balozi Sefue kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda. Baada
ya kupigiwa muda mrefu aliandika ujumbe mfupi wa simu ukisema. “Nimebanwa na majukumu siwezi kupokea simu yako,” ulisomeka ujumbe huo.
Tukio
hilo la CAG limekuja siku mbili baada ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza
kusimamishwa kazi kwa watumishi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU) kwa kosa la kusafiri nje ya nchi bila kibali cha
Ikulu.
Watumishi
wa taasisi hiyo waliosimamishwa kazi ni Ekwabi Mujungu (Mkurugenzi wa
Utawala na Rasilimali Watu), Doreen Kapwani, Rukia Nikitas na Mary
Mosha.
Profesa Assad aliteuliwa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Novemba 5, 2014.
Kabla
ya uteuzi wake, alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam na alichukua nafasi ya Ludovick Utouh ambaye alistaafu
kwa mujibu wa sheria.
Credit: Mtanzania
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni