ZAIDI ya wanafunzi 500 waliochaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza katika Shule mbali mbali za Sekondari Wilayani Chunya Mkoani
Mbeya wameshindwa kuripoti Mashuleni kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo
kujiingiza katika biashara za uchimbaji wa Madini na Uvuvi.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Chunya,
Deodatus Kinawiro, amewataka Wazazi wa Wanafunzi hao kuhakikisha wanawapeleka
watoto wao Shuleni haraka kabla ya kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa mzazi
atakayekaidi agizo hilo.
Kinawiro aliyasema hayo hivi karibuni wakati
akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Majengo kata ya Sangambi Wilayani humo
baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Afisa elimu wa Wilaya kuhusu kukithiri kwa
utoro wa wanafunzi mashuleni, Hivyo kuifanya Serikali kushindwa kufikia malengo
yake ya kufuta ujinga miongoni mwa wananchi.
Alisema Wilaya ya Chunya inakabiliwa na Wimbi
kubwa la wafugaji wenye tabia ya kuhamahama jambo ambalo husababisha
kuwakatisha masomo wanafunzi ili hali wengine wakijikita kwenye shughuli za
uchimbaji wa madini na uvuvi katika Ziwa Rukwa.
Alisema kufikia Mwishoni mwa mwezi huu mzazi
yeyote ambaye hatampeleka Mwanaye Shule bila kujali kisingizio cha aina yoyote
atakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kumwachisha masomo
mwanafunzi na kumpatia ajira kinyume cha Sheria.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema Idadi ya watoto 500
ni kubwa sana hivyo hali hiyo ikiachwa itazalisha Wajinga wengi jambo ambalo
litakuwa mzigo kwa taifa kutokana na wengine kuwa majambazi baada ya kukosa
fedha kutokana na ajira walizojiingiza katika umri mdogo na kukwamisha juhudi
za Serikali za kujenga Shule katika kila kata.
Kinawiro alisema Wilaya ya Chunya kitaaluma
inafanya Vizuri katika ngazi ya Mkoa ukilinganisha na Wilaya zingine hivyo
hayuko tayari kuona sifa hiyo inapotea kutokana na wazazi wachache kuzembea na
kutokujua umuhimu wa kumsomesha mtoto, na kuongeza kuwa Halmashauri inaunga
mkono juhudi za Serikali kwa kuimarisha ujenzi wa Mabweni ili kuhakikisha
watoto wa kike hawakatizwi masomo kutokana na mimba zisizotarajiwa.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka
wafugaji wote waliohamia Wilayani Chunya kinyume cha Sheria kuondoka mara moja
na atakae kaidi agizo hilo atakumbana na Operesheni kubwa ya kuwaondoa kwa
nguvu ambapo kwa sasa wanafanya doria kwa kutumia ndege maalumu ili kuwabaini
wahamiaji hao.
Alisema zoezi hilo litafanyika hivi karibuni
baada ya kumalizi kuwabaini wafugaji waliovamia misitu na sehemu za hifadhi
ambapo wanaharibu kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mifugo ambayo huharibu
mazingira ya Chunya kwa Ujumla.
Hivi karibuni kulifanyika zoezi la kuwaondoa
wafugaji waliovamia msitu wa hifadhi wa kijiji cha Mbangala ambapo Jumla ya
mifugo 1000 ilikutwa msituni humo na kufanyika uharibifu mkubwa lakini zoezi
hilo liliingiliwa na hitilafu baada ya wafugaji hao jamii ya Wamang’ati
kuwashambulia kwa mishale na mikuki maofisa pamoja na Askari wa Jeshi la Polisi
waliokimbia kunusuru maisha yao.
Na E . Kamanga Chunya
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni