Jumamosi, 10 Januari 2015

WENYEVITI WA MITAA JIJI LA MBEYA WAAPISHWA, WALILIA MISHAHARA.



Kaimu Mwanasheria wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Crispin Kaijage akitoa ufafanuzi kwa Wenyeviti wa Mitaa na Wajumbe wao kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Mbeya.

Mmoja wa Wenyeviti wa mitaa akiuliza swali ukumbini hapo kabla ya kuapishwa.


Wajumbe na Wenyeviti wakiwa ukumbini wakisubiri kula kiapo cha kuwatumikia wananchi kwa uaminifu.



Wajumbe wakitoka ukumbini.


Wajumbe wakigawana fomu za viapo.


Wajumbe wakiwa nje ya ukumbi.
  





WENYEVITI wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya wameiomba Serikali kuwaongezea kiwango cha posho ili kiendane na maafisa Watendaji.

Aidha wametoa ombi la wao kutaka kulipwa mishahara kutokana na kuwa wawakilishi wa wananchi na sio kupewa posho jambo ambalo linasababisha wao kudharaulika na watendaji wa Mitaa yao.

Hayo yalitolewa  na Wenyeviti wa Mitaa wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya walipokuwa wakizungumza na Kaimu Mwanasheria wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Crispin Kaijage, kabla ya zoezi la kuwaapisha lililofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mbeya.

Braiton Dibinze Mwenyekiti wa Mtaa wa Kati Kata ya Ruanda alisema kwa mujibu wa Katiba ya nchi sura ya 4 ibara ya 1 hadi ya 3 ya uchaguzi wa serikali za Mitaa, Mwenyekiti wa Mtaa ana ainishwa kama mtawala na mwakilishi wa Raisi katika ngazi ya Mtaa lakini hapewi mshahara kama Watendaji wanaoteuliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri.

Alisema kitendo hicho sio kizuri kwa kuwa wao ndiyo wenye majukumu ya kuhamasisha wananchi kuhusu shughuli za maendeleo hivyo walipaswa kupewa kipaumbele cha malipo tofauti na ilivyo sasa.

“ mimi Mwenyekiti wa Mtaa natambulika kikatiba kama mwakilishi wa Raisi katika ngazi za Mtaa lakini mtu ambaye ajira yake inaishia kwa Mkurugenzi wa Halmashauri analipwa vizuri tunaomba Serikali ilifikirie hilo” alisema Mjumbe huyo.

Kwa upande wake Kaimu Mwanaasheria wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Crispin Kaijage, alisema Mwenyekiti wa Mtaa anapewa Posho ya kila mwezi inayotambuliwa kisheria ambayo ni shilingi 20,000 kwa mwezi sawa na Madiwani ambao pia hupewa posho na sio mshahara.

Aliongeza kuwa kazi ya Mwenyekiti wa Mtaa ni kumsaidia Afisa Mtendaji wa Kata kwa kumsimamia na kumshauri Afisa Mtendaji wa Mtaa kuhusu shughuli za maendeleo pamoja na uwajibikaji wake ili kuondoa ulegevu na kuchelewa maofisini.

“ Ofisi wa Mtaa iko chini ya Afisa mtendaji wa Kata, hivyo tuwe walezi wa Maafisa Watendaji wa Mitaa  pamoja na kuwabana ili wafike maofisini kwa wakati na kutoa taarifa kwa yule anayekiuka utaratibu wa kutekeleza majukumu yake ya kila siku.” Alisisitiza Mwanasheria huyo.

Alisema kitendo cha kuwaapisha viongozi hao kinawapelekea kufanya kazi za serikali katika ngazi za Mitaa wakishirikiana na Maafisa Watendaji kwa mujibu wa sheria na sio kufanya shughuli za kichama.

Mwisho.
Na Mbeya yetu

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni