RAIS mstaafu Benjamin Mkapa, amesema yuko tayari kutoa ushirikiano wa
kila aina au kufanya kazi yoyote endapo Rais Dk. John Magufuli
atahitaji.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Mkapa alitoa
kauli hiyo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo Ikulu na Rais
Magufuli.
Ilisema lengo la Mkapa kukutana na Rais Magufuli ni kumpongeza kwa
dhamana aliyopewa na Watanzania kuiongoza nchi, kuunda Serikali na
kumtakia heri ya mwaka mpya.
“
Mkapa amemhakikishia Rais Magufuli kuwa yupo tayari kutoa
ushirikiano wakati wote ama kufanya kazi yoyote endapo atahitajika
kufanya hivyo,” ilisema taarifa hiyo.
Pia Rais Magufuli alikutana na Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba
ambaye alisema Watanzania wote wanapaswa kumuunga mkono kiongozi huyo
kwa kazi kubwa anazofanya ambazo ni kukomesha rushwa, ufisadi, matumizi
mabaya ya madaraka na wizi wa mali za umma.
“
Lazima kila mmoja amuunge mkono Rais, tusije tukamuachia, pale ulipo
kama ni mambo ya rushwa uanzie hapo hapo, mambo ya matumizi mabaya ya
madaraka anzia hapohapo, tusije tukamuachia Rais peke yake… yeye awe
kiongozi wetu, lakini Watanzania wote tushughulike na matatizo hayo,” ilisema taarifa hiyo ikimkariri Jaji Warioba.
Pamoja na kumtakia heri ya mwaka mpya, Jaji Warioba alimpongeza Rais
Magufuli kwa jinsi alivyoanza kazi vizuri, hususani katika kusimamia
ukusanyaji wa mapato, kubana matumizi na kuelekeza matumizi kwenye
maeneo muhimu ambayo yanawahusu wananchi ikiwamo afya na maji.
Kauli ya Mkapa na Jaji Warioba imekuja siku moja tu baada ya juzi Rais
mstaafu Jakaya Kikwete kumtembelea Rais Magufuli Ikulu na kufanya naye
mazungumzo ambayo hata hivyo yameendelea kuwa ni siri.
Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi wastaafu ndani ya siku mbili
kumtembelea Rais Magufuli tangu ameingia Ikulu Novemba 5, mwaka jana.