Jumamosi, 6 Septemba 2014

Mwanasheria mkuu wa Zanzibar ajitoa katika uandishi wa Katiba



Taarifa ambazo bado hazijathibitishwa ni kwamba mwanasheria mkuu wa Zanzibar amemwandikia barua spika wa bunge la katiba kumtaarifu kujitoa katika timu aliyoiteua kuandika katiba baada ya vifungu kupitishwa na wabunge ambapo kwa kiasi kikubwa wamepingana na rasimu yenye maoni ya wananchi kitu kinachomfanya mwanasheria mkuu huyo kujitoa kwakuwa ni dhambi kuondoa maoni ya wenye nchi yao wananchi.
................................................. 

Dodoma. Kuna dalili hali si shwari ndani ya Bunge Maalumu la Katiba baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kujiuzulu ujumbe wa Kamati ya Uandishi wa Katiba inayopendekezwa.

Habari za uhakika zilizopatikana jana bungeni mjini Dodoma, zinaeleza kuwa kigogo huyo wa SMZ amemwandikia barua Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta akimwarifu juu ya uamuzi wake huo.

Kamati hiyo ndiyo moyo wa Bunge hilo katika kuandika vifungu, ibara na sura za rasimu kulingana na mapendekezo ya kila kamati na baada ya majadiliano na mwisho inawajibika kuandika Katiba itakayopendekezwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

Kujiengua kwake ni pigo kwa Bunge Maalumu, kwani kunapunguza uhalali wa Katiba itakayopendekezwa kwani Othman akiwa Mwanasheria Mkuu wa upande huo wa Muungano ndiye anayepaswa kuwa kinara wa kulinda masilahi ya Zanzibar wakati wa uandishi wa Katiba inayopendekezwa.

Jana Othman alilithibitishia gazeti hili kuhusu kujiuzulu kutoka kwenye kamati hiyo, lakini akakataa kueleza sababu zilizomsukuma kuchukua uamuzi huo akitaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu atafutwe kwani barua yake ya kujiuzulu ameikabidhi kwake.

“Ni sahihi kwamba nimejiuzulu…hizo sababu ndiyo siwezi kukutajia maana kwa mujibu wa taratibu za Bunge Maalumu zinapaswa kuzungumzwa na Mwenyekiti maana barua yangu ya kujiuzulu anayo yeye,”alisema Othman alipozungumza na gazeti hili kupitia simu yake ya mkononi jana.

Hata hivyo, Sitta alipotafutwa jana, alikataa kuzungumza lolote juu ya taarifa hizo akisema hawezi kufanya mahojiano na mwandishi asiyemfahamu kwa njia ya simu.

“Kwanza sikujui halafu unataka nifanye mahojiano kwenye simu? Mimi sipo (Dodoma), nipo Dar es Salaam ninarudi Jumatatu niliondoka huko (Dodoma) mara tu baada ya kipindi cha asubuhi,” alisema Sitta.

Kwa upande wake, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad, alipotafutwa alisema hajaiona barua hiyo ya Othman, lakini kwa utaratibu, mjumbe anayetaka kuchukua uamuzi kama huo humwandikia barua mwenyekiti ndipo ishuke chini.

“Mimi bado sijapata taarifa hiyo, labda atakuwa amewasilisha kwa mwenyekiti akishaipata ndiyo inaletwa huku kwangu,”alisema Hamad.

Alisema kwa sababu nafasi hizo ni uteuzi unaofanywa na mwenyekiti na kanuni ziko kimya kuhusiana na idadi ya wajumbe katika kamati, mwenyekiti ndiye mwenye uamuzi wa kuteua mtu mwingine ama kuacha.


Chanzo: Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni