Jumanne, 13 Mei 2014

RWANDA YAMKATAA BAROZI MTEULE NDG. MUSSA SIWA WA TANZANIA



Rwanda imemkataa Balozi mteule wa Tanzania, Mussa Siwa, ambaye alitakia na serikali kwenda kufanya kazi kwenye ubalozi wa Tanzania nchini humo.Taarifa kutoka Rwanda na duru za ndani ya serikali ya Tanzania zimeeleza serikali ya nchi hiyo imemkataa balozi huyo kwasababu mbalimbali zikiwemo za kiusalama.

Habari kutoka ndani ya Ikulu ya Rwanda zinaeleza kuwa serikali ya nchi hiyo imemkataa balozi Siwa, baada ya kumshuku kuwa ni jasusi. Siwa kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, alikuwa ofisa katika ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani.

Tazania kwa sasa haina balozi nchini Rwanda tangu Dr.Marwa Matiko amalize muda wake wa kufanya kazi hiyo. Nafasi hiya kwa sasa inakaimiwa na Francis Mwaipaja,ambaye kabla ya kupelekwa Rwanda alikuwa msaidizi wa katibu mkuu kiongozi, Ombeni Sefue.

Ofisa mmoja mwandamizi wa Ikulu ya Rwanda aliliambia MTANZANIA kuwa viongozi wa nchi hiyo wanachukuwa tahadhari dhidi ya wanadiplomasia wa Tanzania wanaofanya kazi nchini Rwanda , tangu nchi hizi mbili ziingie katika vita ya maneno mwaka jana.


‘’Viongozi hapa wamekuwa na hofu kubwa na Tanzania na kufanya wawe macho na watanzania wanaoishi hapa na hasa maofisa ubalozi na ndio maana wamemkataa balozi huyo mteule’’. Alisema mtoa taarifa wetu.

Wafuatiliaji wa maswala ya kidiplomasia wametafsiri kitendo hicho kuwa ni mwendelezo wa kutofautiana kati ya serikali za nchi hizi mbili.

Rwanda iliingia katika mgogoro na Tanzania baada ya kuchukizwa na ushauri uliotolewa na Raisi Jakaya Kikwete wa kuitaka serikali ya nchi hiyo kufanya mazungumzo na kundi la waasi la FDLR, ambalo limejichimbia ndani ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Rais kikwete alitoa ushauri huo mbele ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Kin-Moon na Raisi wa Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma, wakati wa mkutano wa viongozi wa ukanda wa maziwa makuu ya afrika uliofanyika mjini Addis Abab, Ethiopia, Mei, mwaka jana.

Ushauri huo ulipokelewa vibaya na Rais Kagame na waziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi hiyo, Louise, Mushikiwabo, ambao walitoa kauli za kumdhalilisha Rais Kikwete.


Mkataba wa Vienna

Hata hivyo, Rwanda ina uhuru wa kisheria wa kumkataa balozi mteule wa kigeni kama inaona hafai kwenda kuishi nchini humo. Kifungu cha nne cha mkataba wa kimataifa wa Vienna wa mwaka 1961 unaozungumzia masuala ya kidiplomasia baina ya mataifa,kinatoa uhuru wa nchi kumkubali balozi mteule wa kigeni. Mathalani Tanzania , mwaka jana ilimkataa balozi mteule wa Ujerumani, Margit Hellwig – Boette, ambaye alitakiwa kuja kuwa balozi hapa nchini mara baada ya kumaliza muda wake nchini Kenya.

Sefue asema hana taarifa

Akizungumzia suala hilo, Sefue alisema taarifa hizo hajazipata na kwamba wizara ya mambo ya nje ndiyo inayoweza kufahamu vizuri suala hilo. ‘’Mimi sifahamu chochote kwakweli, nadhani watu wa wizara ya mambo ya nje ndiyo wanajua process (taratibu) hizi ndiyo maana hata jina la huyo balozi aliyekataliwa silijui’’ alisema.

Wizara ya mambo ya nje washangaa

Nae mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, Mkumbwa Ally, alishangaa na kuhoji kuwa hizo taarifa tumezipata wapi kwani ni habari za ndani.

‘’Hizo taarifa mmezipata wapi, ni taarifa za ndani, chanzo chako cha habari ni nani’’,alihoji ally. Hata hivyo, alipoombwa kuzungumzia swali la msingi alisema suala hilo lipo nje ya uwezo wa wizara yake kwani Rais Kikwete ndiye mwenye mamlaka ya kuteuwa na kutangaza jina la mteule huyo.

“Kiujumla sijapata taarifa za uhakika kuhusu suala hilo kwa sababu uteuzi wa balozi yeyote ni ‘process’ utaratibu’’ , hivyo hatuwezi kujua jina lake mpaka uteuzi wake ukamilike ndipo tutangaziwe na mwenye mamlaka hayo ni Rais, hivyo siwezi sema chochote ‘’
alisema.

MTANZANIA lilifanya jitihada za kumtafuta Siwa bila mafanikio kuzungumzia suala hilo.

Katika siku za hivi karibuni uhusiano baina ya Tanzania na Rwanda umeonekana kusuasua na hata viongozi wa nchi hizi mbili wamekuwa wakidaiwa kukwepana katika hafla mbalimbali zinazohusu nchi zao pamoja na zile za jumuiya ya Africa mashariki(EAC).

Wiki mbili zilizopita, Rais kagame alikacha kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na zanzibar zilizofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na marais wote wanachama wa ( EAC).

Mbali na Kagame kutokuhudhuria maadhimisho hayo, pia aliukacha mkutano wa wakuu wa nchi za EAC uliofanyika jijini Arusha, lakini alikwenda nchini Kenyana kuhudhuria kikao cha viongozi wa nchi za Afrika Mashariki wanaounganishwa na mradi unaoitwa ‘ Northern Corridor Infrastructure Project’. Waziri Mkuu Pinda aliiwakilisha Tanzania katika mkutano huo.


Source: Gurudumu la Habari 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni